Tanga, Tanzania – Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetekeleza operesheni ya mafanikio usiku wa tarehe 22 Julai 2025 kwa kukamata boti aina ya fibre, rangi nyeupe, iliyokuwa ikisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka nchini Kenya kupitia Bahari ya Hindi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi, amethibitisha kukamatwa kwa boti hiyo katika eneo la Mawe Mawili, Kijiji cha Kwale, lililopo mpakani mwa Wilaya ya Mkinga na Jiji la Tanga.
Kamanda Mchunguzi alieleza kuwa operesheni hiyo ilifanikishwa na Kikosi cha Polisi Wanamaji (Marine Police) kufuatia taarifa za kiintelijensia pamoja na ufuatiliaji wa kina wa mbinu zinazotumiwa na wasafirishaji haramu wa dawa za kulevya.
“Watuhumiwa wawili waliokuwa ndani ya boti hiyo walifanikiwa kutoroka baada ya kufika karibu na fukwe, hata hivyo boti pamoja na shehena ya mirungi ilikamatwa na ipo mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi,” alisema ACP Mchunguzi.




Kamanda huyo aliongeza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linaendelea kuimarisha doria na operesheni maalum, hususan katika maeneo ya baharini ambayo yamekuwa yakitumika kama njia za usafirishaji haramu wa bidhaa kutoka nchi jirani.
Aidha, aliwataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za mapema kuhusu vitendo vyovyote vya uhalifu, hasa vinavyohusiana na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.
“Ushirikiano wa wananchi ni silaha muhimu katika vita dhidi ya dawa za kulevya. Tunawaomba muendelee kutuamini na kutoa taarifa kwa wakati,” alisisitiza Kamanda Mchunguzi.
Tukio hili linaongeza msisitizo juu ya umuhimu wa ulinzi madhubuti katika maeneo ya mipakani na baharini, ambapo mitandao ya kihalifu imekuwa ikijaribu kutumia mianya hiyo kuingiza dawa za kulevya ndani ya nchi.



