Rais Samia atembelea Makumbusho ya Rais wa kwanza wa Angola, Hayati António Agostinho Neto

Luanda, Angola – Aprili 8, 2025


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ametembelea Makumbusho ya Rais wa Kwanza wa Angola, Hayati António Agostinho Neto, yaliyopo eneo la Public Square, jijini Luanda.

Katika ziara hiyo ya kihistoria, Rais Samia alipokelewa kwa heshima ya kijeshi, ikiwa ni ishara ya urafiki na heshima baina ya mataifa haya mawili rafiki. Baada ya mapokezi hayo rasmi, aliweka shada la maua katika Mnara wa Kumbukumbu wa Hayati Neto, kuenzi mchango wake mkubwa katika harakati za ukombozi wa Angola na Afrika kwa ujumla.

Hayati António Agostinho Neto alikuwa kiongozi wa kwanza wa taifa huru la Angola na mmoja wa mashujaa waliopigania uhuru wa mataifa ya Kiafrika dhidi ya ukoloni. Ziara hii ya Rais Samia ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Angola.

Tukio hili pia linaashiria msimamo wa Tanzania wa kuendelea kuthamini na kuheshimu viongozi waasisi wa uhuru wa Afrika, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya maendeleo, amani na mshikamano wa bara la Afrika.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *