RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha kubwa la michezo na burudani la ‘Grand Bunge Bonanza’, linalotarajiwa kufanyika kesho, Juni 21, 2025 Jijini Dodoma.

Tamasha hilo litaambatana na matembezi maalum ya afya yatakayoanzia Chuo cha Mipango hadi viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlini jijini hapa, pamoja na tamasha la nyama choma, likiwa na lengo la kuhamasisha afya bora na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kupokea msaada wa vifaa vya michezo kutoka Benki ya CRDB, Mwenyekiti wa Timu ya Bunge Sports Club, Festo Sanga, alisema bonanza hilo linahitimisha mabonanza ya Bunge la 12 ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.
“Mwaka huu bonanza litakuwa la kipekee zaidi kwani linakuja siku chache kabla ya Bunge kufungwa rasmi na Rais. Tumeamua kuwa pamoja naye ili kuonesha mshikamano, umoja na kufunga pazia kwa pamoja,” alisema Sanga.
Aidha, alieleza kuwa CRDB ikiwa mdhamini mkuu, imetoa msaada wa vifaa vyote vya michezo na itashirikisha baadhi ya taasisi jijini humo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa benki hiyo, TullyEsther Mwampamba, alisema benki hiyo imetoa msaada wenye thamani ya Sh. milioni 130 kwa ajili ya michezo hiyo, ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii kupitia sekta za elimu, afya na michezo.
“Tunataka Dodoma irindime kwa hamasa na mshikamano. Kupitia Bonanza hili tunatimiza dhamira yetu ya kuchangia maendeleo ya jamii,” alisema Mwampamba.