Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema mshikamano wa wachezaji wake katika kushambulia na kuzuia pamoja bila kutegeana ndiyo sababu ya mafanikio ya timu hiyo.

Akizungumza baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Ramovic alisisitiza kuwa bado wanajipanga kuwa na utimamu wa mwili kwa asilimia 100 ili kucheza kwa kasi kwa dakika zote 90.
Yanga imeendelea kung’ara chini ya Ramovic, ikishinda michezo minne mfululizo huku ushindi huo ukiwabakisha katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 36, nyuma ya vinara Simba wenye pointi 37.
Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime, alikubali kipigo hicho, akisema makosa ya wachezaji wake yaliwapa Yanga nafasi ya kuwatandika mabao manne.
Yanga sasa inajipanga kwa mechi dhidi ya Fountain Gate na TP Mazembe katika Ligi ya Mabingwa Afrika Januari 3, mwakani.