Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amewataka waajiri na waajiriwa kuhakikisha wanazingatia nidhamu, maadili na utawala bora katika maeneo ya kazi ili kuweka uwiano mzuri kati ya wafanyakazi na viongozi wao.

Amesema nidhamu kazini, maadili na utumishi uliotukuka ni mambo ya msingi ambayo viongozi na wakuu wa taasisi wamekuwa wakiyasimamia kwa umakini kwa watumishi wao, huku akisisitiza kuwa suala hilo haliwahusu watumishi pekee, bali pia viongozi wanaosimamia taasisi hizo.
Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa 66 wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Waziri Ridhiwani amesema usimamizi mzuri unaozingatia sera za utumishi na utawala bora ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele si Serikalini tu bali pia katika sekta binafsi.

Awali, akitoa taarifa yake katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran, alisema pamoja na mambo mengine, chama hicho kinaendelea kuishauri Serikali kufanya maboresho ya sheria zinazohusiana na waajiri ili kuweka usawa wa kiutendaji kati ya waajiri na waajiriwa.









