Dar es Salaam, Tanzania – 31 Julai 2025: Mavuno hafifu yanayosababishwa na matumizi ya mbolea na viuatilifu bandia, mabadiliko ya ghafla ya mvua, ukosefu wa ujuzi wa kilimo cha kisasa, pamoja na matumizi ya teknolojia zilizopitwa na wakati, ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokwamisha uzalishaji wa mazao nchini Tanzania.

Haya ndiyo masuala makuu ambayo mpango wa Serengeti Breweries Limited (SBL) wa ‘Shamba ni Mali‘ uliozinduliwa leo unalenga kuyashughulikia, ikiwa ni sehemu ya dhamira mpya ya kampuni kuboresha maisha ya maelfu ya wakulima wa ndani ambao SBL hununua kutoka kwao mahindi, mtama na shayiri yanayotumika katika uzalishaji wa bia.
“Mpango wa ‘Shamba ni Mali‘ unalenga kuwanufaisha moja kwa moja zaidi ya wakulima wadogo 4,000 kote nchini, hasa wale wanaolima mtama, shayiri na mahindi. Mpango huu umeundwa kuwawezesha wakulima kwa kuwapatia soko la uhakika la mazao yao, upatikanaji wa mbegu bora zenye tija kwa shayiri na mtama, na mafunzo muhimu juu ya kanuni bora za kilimo, ikiwemo kilimo kinachojali mazingira,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi.
Obinna anaongeza kuwa mpango huo unalenga kuongeza thamani ya biashara kwa kununua malighafi kwa njia endelevu ili kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa wa uhakika, kuimarisha uthabiti na kulinda sifa nzuri ya biashara, huku ukiwahakikishia faida wakulima na kuboresha maisha yao kote nchini.
Mpango wa ‘Shamba ni Mali‘ pia utazingatia kujenga uhusiano imara na wakulima kupitia ziara za mara kwa mara za wataalamu kwa ajili ya kubadilishana maarifa na kuendeleza mikutano ya mara kwa mara na wakulima. Kitu kingine muhimu katika mpango huu ni biashara jumuishi, kwa kuwawezesha wanawake, vijana, na makundi yaliyotengwa kwa kushiriki katika mikataba rasmi na kupata huduma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, alisema, “Mpango wa ‘Shamba ni Mali’ unaendana vyema na Mpango Mkuu wa Kilimo Tanzania 2050, wenye maono yanayolenga kubadilisha sekta ya kilimo nchini kuwa endelevu, imara, na jumuishi ifikapo mwaka 2050, na hivyo kuiweka Tanzania kama nchi ya kipato cha kati cha juu.”
Uzinduzi wa mpango huo uliwakutanisha wadau muhimu kutoka Serikalini, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wadau wengine kutoka sekta ya kilimo.
Kuhusu SBL:
Ikianzishwa mnamo mwaka 1988 kama Associated Breweries, SBL ni kampuni ya pili kwa ukubwa kwa utengenezaji wa bia nchini Tanzania, huku chapa zake za bia zikichukua zaidi ya asilimia 25 ya soko. SBL ina viwanda vitatu vya uzalishaji vilivyopo Dar es Salaam, Mwanza na Moshi. Tangu kuanzishwa kwa SBL mwaka 2002, biashara imeongeza idadi ya chapa zake mwaka hadi mwaka. Ununuzi wa hisa nyingi na EABL/Diageo mnamo 2010 umepelekea kuongezeka kwa uwekezaji katika viwango vya kimataifa vya ubora na kusababisha fursa zaidi za ajira kwa Watanzania. Chapa za SBL zimekuwa zikipokea tuzo nyingi za kimataifa ambazo zinajumuisha Serengeti Premium Lager, Serengeti Lite, Serengeti Lemon, Pilsner Lager, Kibo Gold, Guinness Stout na Senator. Kampuni hiyo pia inazalisha vileo mashuhuri duniani kama Johnnie Walker Whisky, Smirnoff Vodka, Gordon Gin, Captain Morgan Rum na Baileys Irish Cream.