Serikali yazindua mwongozo wa kutokomeza utumikishwaji wa watoto kwenye Kilimo

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imezindua Mwongozo wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Watoto katika Sekta ya Kilimo, ukiwa na lengo la kuimarisha utekelezaji wa sheria za kazi na kulinda haki za watoto.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi, Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa, alisema takwimu za mwaka 2024 zinaonesha watoto takriban milioni 5 (asilimia 25) wanajihusisha na kazi, huku milioni 4.9 wakiwa kwenye ajira mbaya, asilimia 84.1 kati yao wakiwa katika sekta ya kilimo.

“Mwongozo huu unaweka mwelekeo mahsusi kwa wadau wa kilimo, kuongeza kasi ya kupambana na ajira za watoto,” alisema Mkangwa.

Alibainisha kuwa Serikali itaendesha mafunzo kwa wadau wa msingi ili kuhakikisha mwongozo unasambazwa katika ngazi zote za Serikali Kuu na Mitaa, sambamba na kaguzi, elimu na ushauri.

Mpango kazi maalum kwa kila mdau umeandaliwa ili kufuatilia utekelezaji na utoaji wa taarifa kwa mamlaka husika.

Aidha, Mkangwa aliipongeza Wizara ya Kilimo, Bodi za Mazao na Shirika la ECLT kwa mchango mkubwa katika kusimamia haki za wafanyakazi, hususan katika sekta ya tumbaku na kilimo kwa ujumla.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *