Klabu ya Simba imeingia mkataba mpya wa miaka mitano na kampuni ya Jayrutty Investment, wenye thamani ya Shilingi bilioni 38, ambao unaihakikishia klabu hiyo mapato ya takriban Shilingi bilioni 8 kwa mwaka.

Kupitia mkataba huo, Simba itapokea Sh bilioni 7.6 kila mwaka pamoja na nyongeza ya Sh milioni 570 kwa ajili ya posho, motisha kwa wachezaji, na maandalizi ya Simba Day.
Jayrutty Investment imeshinda zabuni ya kuzalisha na kusambaza bidhaa zote za klabu hiyo, ikiwemo jezi za msimu ujao, kuchukua nafasi ya kampuni ya Sandaland waliokuwa na mkataba wa Sh bilioni 4 kwa miaka miwili.
Mbali na vifaa vya michezo, mkataba huo pia unahusisha ujenzi wa uwanja wa kisasa utakaoingiza mashabiki 10,000–12,000 na ununuzi wa basi jipya aina ya Irizar. Jayrutty pia itaongeza Sh milioni 100 kila mwaka kwa ajili ya Simba Day.
Waziri wa Michezo, Hamis Mwinjuma, aliipongeza Simba kwa kufanikisha mchakato wa kisasa wa zabuni hiyo na kuitakia mafanikio katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini.