Simba yafaidika na uwanja kuamishwa dhidi ya Al Masry

Timu ya Simba SC inanufaika na uamuzi wa mamlaka za soka nchini Misri wa kuhamishia mchezo wao wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) dhidi ya Al Masry kwenye mji wa Suez badala ya Ismailia, uwanja wa nyumbani wa wapinzani wao.

Mratibu wa Simba, Abbas Ally, amesema mamlaka hizo zimehamishia mechi hiyo Suez kutokana na ukorofi wa mashabiki wa Al Masry, ambao wamewahi kusababisha vurugu kwenye michezo kadhaa. Ingawa Ismailia na Suez ziko umbali wa kilomita 80, uamuzi huo unatarajiwa kupunguza presha kwa Simba kwani mashabiki wa Al Masry hawatakuwa wengi kama wangekuwa nyumbani kwao.

Simba pia imenufaika kwa kuruhusiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja wa kisasa wa Suez Canal Authority, ambao hutumiwa kwa mechi kubwa pekee. Abbas amesema uwanja huo ni wa viwango vya juu barani Afrika na si kila timu inaruhusiwa kuutumia kwa mazoezi.

Kikosi cha Simba kitaondoka Ismailia Jumanne kwa maelekezo ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids, ambaye anataka timu ifanye mazoezi kwenye uwanja wa mechi siku moja kabla ya mchezo, utakaopigwa Jumatano saa 1:00 usiku. Mchezo wa marudiano utafanyika Aprili 9, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *