Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids, amesema kikosi chake kimewasili Afrika Kusini kwa kazi moja tu—kuhakikisha kinatinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza jijini Durban baada ya kutua kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Stellenbosch FC Jumapili hii, Fadlu amesema hana hofu yoyote na amejiandaa kikamilifu kuhakikisha Simba inafanikiwa.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Zanzibar, Simba ilishinda bao 1-0, hivyo inahitaji sare yoyote au ushindi ili kufuzu fainali. Fadlu amesema kuwa ujio wao nchini humo ni wa kutekeleza mpango wa kuandika historia, huku akiwataka Watanzania na washabiki wa soka Afrika Kusini kujitokeza kwa wingi kuishangilia Simba.
Kwa upande wake, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema timu hiyo tayari imeanza mazoezi, ikiwemo gym mara baada ya kuwasili, ili kuwaweka wachezaji fiti na kuzoea hali ya hewa ya baridi na mvua ya Durban. Pia amesema Stellenbosch haina mashabiki wengi katika jiji hilo, hivyo Simba inaweza kugeuza uwanja huo kuwa kama nyumbani.
Ahmed amesema mashabiki wa Simba kutoka nchi za Afrika Kusini na Afrika Mashariki wamehamasishwa kufurika uwanjani Jumapili. Simba inahitaji ushindi au sare ili kufuzu, huku ikitarajia kutumia uzoefu wake na morali nzuri ya ushindi wa awali kumaliza kazi.