Singida Black Stars wameandika historia kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame 2025 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan, katika fainali iliyochezwa leo Septemba 15, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Shujaa wa mchezo huo alikuwa kiungo raia wa Zambia, Clatous Chama, aliyefunga mabao yote mawili yaliyoipeleka Singida Black Stars kwenye taji hilo la kihistoria. Chama alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 20, kabla ya Al Hilal kusawazisha kupitia Taha Abdelrazig dakika ya 31, na kufanya matokeo kuwa 1-1 hadi mapumziko.
Katika kipindi cha pili, Singida Black Stars walionesha uimara na ari kubwa, na jitihada zao kufanikiwa baada ya Chama kupachika bao la pili lililowapa ubingwa wa kwanza wa michuano hiyo tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo.

Kwa ushindi huo, Singida Black Stars wamejiunga na orodha ya timu za Tanzania zilizowahi kutwaa Kombe la Kagame, zikiwemo Simba, Yanga na Azam.
Baada ya mchezo, Clatous Chama alinyakua tuzo mbili kubwa: Mchezaji Bora wa Mechi na Mfungaji Bora wa Mashindano, huku kipa Metacha Mnata akiibuka mshindi wa tuzo ya Kipa Bora.
Ushindi huu umetajwa na wadau wa soka kama ishara ya kupanda kwa kiwango cha Singida Black Stars na nguvu ya klabu za Tanzania katika medani ya soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.








