Klabu ya Singida Black Stars imetangaza kufanya mabadiliko mbalimbali katika safu ya uongozi wa timu hiyo, yakiwemo mabadiliko katika benchi la ufundi, hatua inayolenga kuimarisha utendaji na mafanikio ya klabu hiyo.
Katika mabadiliko hayo, Kocha Miguel Gamondi ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu, nafasi ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Ramadhan Nsanzurwimo, ambaye sasa atahudumu kama Mshauri wa Ufundi wa Singida Black Stars.
Sambamba na hilo, klabu hiyo imemtangaza David Ouma raia wa Kenya kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho. Ouma atasaidiwa na makocha wasaidizi Mousa Nd’aw pamoja na Muhibu Kanu, ambao kwa pamoja wanatarajiwa kuimarisha benchi la ufundi na ushindani wa timu.
Aidha, Singida Black Stars imemwajiri Othmen Najjar kuwa Meneja Mkuu wa klabu hiyo, hatua inayolenga kuimarisha mifumo ya uendeshaji na usimamizi wa shughuli za kila siku za klabu.
Mabadiliko hayo yanaonyesha dhamira ya Singida Black Stars ya kuwekeza katika uongozi imara na benchi la ufundi lenye uwezo, kuelekea msimu ujao wa mashindano.




