Suluhisho nishati safi kupikia lapamba moto Tanzania

Katika majiko mengi Tanzania, tendo la kuandaa chakula si jambo la kawaida tena, bali ni desturi ya kila siku iliyosheheni katika maisha ya kila familia na jamii nzima. Hata hivyo, nyuma ya mambo yote kuna uhalisia kuwa mazoea haya hayajapata tathmini vizuri, ikizingatiwa ya kuwa bado kuna mamilioni ya watanzania wanategemea nishati ya kuni na mkaa — vyanzo vinavyohatarisha afya, kuharibu mazingira, na kuongeza mzigo wa kiuchumi.

Takwimu zinaeleza hali ya kushtusha. Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kaya nyingi nchini bado zinatumia kuni na mkaa kama vyanzo vya nishati ya kupikia. Hali hii ina athari pana. Moshi wa ndani unaotokana na kuchoma kuni na mkaa ni chanzo kikuu cha maradhi ya mfumo wa upumuaji, hasa kwa wanawake na watoto wanaokaa karibu na maeneo ya kupikia kwa muda mrefu. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria watu takribani milioni 3.2 hufariki kila mwaka duniani kutokana na magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa majumbani.

Mzigo wa kiuchumi pia ni mkubwa. Kwa mujibu wa utafiti wa Benki ya Dunia wa mwaka 2023, kaya za mijini nchini Tanzania hutumia hadi asilimia 30 ya kipato chao kununua mkaa, huku familia za vijijini zikitumia muda na nguvu nyingi kukusanya kuni. Zaidi ya hapo, matumizi makubwa ya kuni na mkaa yanasababisha uharibifu wa misitu, kuhatarisha mifumo ya ikolojia na kudhoofisha uimara wa tabianchi.

Hata hivyo, Tanzania imeanza safari ya kuelekea kwenye matumizi ya nishati ya kisasa, ikiashiriwa na mafanikio makubwa katika uzalishaji na usambazaji wa umeme. Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, serikali imewekeza kwenye miradi mikubwa ya miundombinu ya nishati ili kuongeza upatikanaji wa umeme. Miongoni mwa maendeleo haya ni Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115, na hivyo kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kitaifa wa umeme. Uwekezaji wa ziada katika mitambo ya gesi na umeme wa jua unaongeza idadi wa vyanzo vya nishati.

Juhudi za kuongeza upatikanaji wa umeme zimeendelea kuimarika. Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umefanikiwa kuunganisha vijiji 12,318 (sawa na asilimia 100) kwenye umeme tangu kuanzishwa kwake, hatua inayoiwezesha Tanzania kufikia malengo ya upatikanaji wa umeme kwa wote ifikapo mwaka 2030. Kadri mchakato wa umeme unavyoendelea kufikia maeneo ya mijini na pembezoni, fursa mpya zinaibuka, ikiwemo kubadili namna ya kupika.

Kupika kwa umeme, au eCooking, ni moja ya maeneo mapya yenye matumaini. Tofauti na mbinu za jadi, eCooking hutumia vifaa kama vile sufuria za shinikizo za umeme, jiko la induction, na rice cooker ambavyo ni safi zaidi, vya haraka na vyenye ufanisi mkubwa. Kadri kaya nyingi zinavyopata umeme wa uhakika, vifaa hivi vinaacha kuwa vya watu wachache na kuanza kupatikana kwa wengi.

Mwelekeo huu wa mabadiliko ulipata msukumo mpya tarehe 2 Juni 2025, serikali ilipozindua Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano Kupikia Nishati Safi 2024–2034 jijini Dodoma. Hatua hii imejengwa juu ya uzinduzi wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupikia Safi (2024–2034) uliofanyika tarehe 8 Mei 2024, unaoelekeza dira ya miaka 10 ya kufanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.

Mkakati huu unasisitiza matumizi ya nishati safi na pia kuhamasisha teknolojia salama kama vile kupikia kwa umeme, hasa kwenye maeneo yenye miundombinu ya umeme. Vilevile, mkakati umeunganisha ajenda ya kupikia safi na ajenda pana za kitaifa za upatikanaji wa umeme, mabadiliko ya tabianchi na afya ya umma — kuhakikisha kuwa hili halibaki kuwa suala la pembeni bali kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.

Katika wiki zijazo, mageuzi haya yanatarajiwa kuonekana zaidi kwa vitendo. Tanzania ipo katika hatua ya kihistoria ya kubadili taswira ya kupika kwa mamilioni ya raia wake. Kwa familia, jamii na taasisi mbalimbali, huu unaweza kuwa mwanzo wa maisha bora zaidi, yenye afya na njia ya kisasa ya kupika na kuishi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *