Morogoro, Oktoba 2025 — Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO SACCOS) kimefanikiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa wanachama wake baada ya kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 27.2 katika kipindi cha miezi minane pekee ya mwaka 2025.
Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO SACCOS, Omari Shaaban, wakati wa Mkutano Mkuu wa 57 wa mwaka, uliofanyika mjini Morogoro.



“Kuanzia Januari hadi Agosti 31, 2025, chama chetu kimetoa mikopo yenye jumla ya Sh 27,257,207,164 kwa wanachama 4,031. Mikopo hii imetolewa kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyowekwa na chama kupitia sera ya mikopo,” alisema Shaaban.
Alisema mikopo hiyo imezingatia tathmini ya uwezo wa mkopaji, upatikanaji wa wadhamini wa kuaminika, na uwezo wa urejeshaji wa kila mwanachama, hatua ambayo imehakikisha uimara wa kifedha wa chama hicho.
Mtaji waongezeka kwa zaidi ya asilimia 75
Shaaban alieleza kuwa mtaji wa chama umeendelea kukua kwa kasi, kutoka Sh Bilioni 4.9 mwaka 2023 hadi Sh Bilioni 7.1 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 75.
Aidha, hisa za wanachama ziliongezeka kwa asilimia 5, kutoka Sh 10.6 Bilioni mwaka 2023 hadi Sh 11.18 Bilioni mwaka 2024.
Vilevile, akiba za wanachama ziliongezeka kutoka Sh 44.7 Bilioni (2023) hadi Sh 46.9 Bilioni (2024), na chama kimeweza kutoa faida ya Sh 907,161,712 juu ya akiba hizo.

TANESCO SACCOS yajali jamii kwa vitendo
Mbali na huduma za kifedha, Shaaban alisema chama hicho kinatekeleza pia msingi wa saba wa vyama vya ushirika unaohimiza vyama kujali na kusaidia jamii inayowazunguka.
Kwa mwaka 2025, chama kimetumia Sh Milioni 23 kuchapisha na kusambaza shuka 1,300 katika hospitali za rufaa na mikoa nchini, ikiwemo hospitali za jiji la Dodoma, huku mpango huo ukiwa endelevu kwa mikoa mingine.
TANESCO yajivunia SACCOS yao
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia uzalishaji, Mhandisi Antony Mbushi, alisema shirika linajivunia mafanikio ya SACCOS hiyo.

“Tunapongeza uongozi wa TANESCO SACCOS kwa kazi nzuri. Tunashauri waendelee kupanua misaada kwa maeneo mengine, si hospitali pekee, bali pia kusaidia makundi yenye mahitaji maalum,” alisema Mbushi.
Wanachama wafurahia mafanikio
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo kutoka Kahama, mkoani Shinyanga, Bw. Wilson Kingu, alisema SACCOS hiyo imekuwa mkombozi kwa wanachama wengi.
“Saccos yetu ni msaada mkubwa. Mimi binafsi ninaweza kupata mikopo mikubwa kwa urahisi na kurejesha kwa utaratibu mzuri. Hii imenibadilishia maisha,” alisema Kingu kwa furaha.
TANESCO SACCOS imeendelea kuwa mfano bora wa vyama vya ushirika nchini vinavyowezesha wanachama wake kujitegemea kiuchumi, sambamba na kuchangia maendeleo ya kijamii kupitia huduma endelevu.