Wizara ya Madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) na Taasisi ya Jiosayansi na Rasilimali Madini ya Korea Kusini (KIGAM) zimetia saini Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya kufanya tafiti za pamoja za jiosayansi.

Hafla hiyo ya utiaji saini ilifanyika Machi 26, 2025, jijini Seoul, Korea Kusini, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa. Ziara hiyo ilihusisha ushiriki wa mkutano wa wadau wa madini mkakati ulioandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara, Viwanda na Nishati ya Korea Kusini pamoja na wadau wa sekta binafsi kutoka Tanzania na Korea Kusini.
Hati hiyo inalenga kushirikiana katika kutekeleza miradi ya pamoja ya utafiti wa jiolojia, jiokemia, na jiofizikia ili kubaini maeneo mapya yenye madini muhimu na madini mkakati.
Maeneo Muhimu ya Makubaliano
Mbali na tafiti za jiolojia, makubaliano hayo yanajumuisha:
- Kuendeleza miradi ya pamoja ya utafiti wa majanga ya asili.
- Kujengeana uwezo wa kitaalam na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa jiosayansi na utafiti wa madini.
- Kufanya tafiti za uchenjuaji wa madini kwa lengo la kuboresha uzalishaji na uongezaji thamani wa madini nchini.
- Kuandaa mifumo madhubuti ya utunzaji wa taarifa za jiosayansi.
- Kuimarisha maabara ya GST kwa kuongeza vifaa na teknolojia za kisasa.




Kabla ya hafla ya utiaji saini, Ujumbe wa Tanzania ulipata nafasi ya kutembelea na kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na KIGAM. Ziara hiyo iliwapa fursa ya kuona teknolojia zinazotumika katika:
- Utafiti wa njia mbalimbali za uchenjuaji wa madini, hususan madini mkakati.
- Utafiti wa teknolojia za utengenezaji wa vifaa vya teknolojia ya kijani, ikiwemo betri za magari ya umeme.
- Utambuzi wa majanga ya asili kama mitetemo ya ardhi na milipuko.
- Kutembelea Chuo cha Jiosayansi na Rasilimali Madini kinachomilikiwa na KIGAM.




Akizungumzia ushirikiano huo, Dkt. Kiruswa aliishukuru Serikali ya Korea Kusini kupitia KIGAM kwa kukubali kushirikiana na Tanzania katika tafiti za jiosayansi na kujenga uwezo wa wataalamu wa Kitanzania. Pia, aliahidi kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo ili kuhakikisha yanaleta manufaa kwa pande zote mbili.
Makubaliano haya yanatarajiwa kuimarisha sekta ya madini nchini Tanzania na kuongeza ufanisi katika uvumbuzi wa madini mkakati kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.

