Tanzania yajipanga kutokomeza polio

TANZANIA imeweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kutokomeza kabisa ugonjwa wa polio, kwa kuhakikisha hakuna visa vipya vitakavyoingia nchini.

Mikakati hiyo imewekwa  na nchi kama njia ya kukabiliana na ugonjwa huo ambao hivi karibuni, umeripotiwa katika nchi za Kenya, Uganda, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia  ya Congo (DRC).

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk. Vida Makundi, aliyasema hayo jana katika Mkutano wa 34 wa siku nne wa Ukanda wa Afrika wa Kutokomeza Ugonjwa wa Polio, jijini Dar es Salaam.

Alisema Tanzania mgonjwa wa mwisho kuripotiwa mwaka 1996 na kuanzia hapo  hakuna aliyebainika,alidai, ili kuudhibiti wanatoa chanjo kwa watoto wote na kufanya ufuatiliaji wa karibu kubaini endapo kuna dalili za ugonjwa huo, kwa watoto chini ya miaka 15 na kukusanya sampuli katika mipaka ya nchi, kugundua maambukizi mapya.

“Katika kikao hiki, tutawaelezea wenzetu mikakati tuliyoweka na wao wajifunze na sisi tutajifunza kutoka kwao, tunaweka nguvu za pamoja kuhakikisha dunia haina Polio 2030,” alisema Dk. Makundi.

Mratibu wa Kutokomeza Polio Kanda ya Afrika, Jamal Ahmed, alieleza kuwa mkutano huo una lengo la kujadili mbinu za kupambana na virusi vinavyosambaa kwa kuvuka mipaka na kuanzisha mikakati ya kukomesha ugonjwa huo ifikapo Desemba, 2025.

Ahmed alisema lengo lao ni kuhakikisha watoto wote katika ukanda wa Afrika wanakuwa salama na kwamba wataweka hatua za dharura za pamoja kuutokomeza ugonjwa huo.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Hafidhi, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, alisisitiza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kuondoa polio, alisema ili nchi iwe salama zaidi, ni muhimu majirani pia  kuongeza juhudi kupambana na ugonjwa huo.

Hafidhi aliongeza kuwa Tanzania inahitaji kuimarisha miundombinu ya maabara na kuongeza ufadhili kwa kampeni za chanjo, ili kuzuia uwezekano wa virusi kuingia tena nchini.



Kiongozi wa huduma za Chanjo na Ufuatiliaji wa Magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk. William Mwengee, alisema Tanzania ilipata cheti cha kutokuwa na polio mwaka 2015.

Alisema WHO inaendelea kushirikiana na nchi hiyo kwa kutoa msaada wa kifedha na kitaalamu, ili kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo na nchi inafuatilia kwa ukaribu dalili zozote za ugonjwa.

“Tumepewa kazi ya kusaidia nchi kitaalamu na kifedha kwanza kuhakikisha uchanjaji kwa watoto wote pili kampeni za chanjo ili kupata watoto wote tulifika kila mahali tatu ni ufuatiliaji wa watoto waliopooza ghafla kwa kuwapima,” alisema Dk. Mwangee.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *