Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemteua Kocha wa Singida Black Stars, Miguel Angel Gamondi, raia wa Argentina, kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania – Taifa Stars, akichukua nafasi ya Hemed Suleiman ‘Morocco’, ambaye mkataba wake umesitishwa kwa makubaliano ya pande zote mbili.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na TFF leo, Novemba 4, 2025, mazungumzo kati ya TFF na uongozi wa Singida Black Stars yamekamilika, na pande zote zimekubaliana kuhusu Gamondi kuchukua majukumu hayo mapya.
Kocha Gamondi, ambaye aliwahi kuinoa Young Africans SC (Yanga), ataiongoza Taifa Stars katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika nchini Morocco kuanzia mwezi Desemba mwaka huu.
TFF imesisitiza kuwa uteuzi huo unalenga kuimarisha maandalizi ya timu ya Taifa kuelekea michuano hiyo mikubwa ya bara la Afrika, huku ikiendelea kuweka mazingira bora ya mafanikio kwa wachezaji na benchi la ufundi.




