Timu ya Taifa ya mchezo wa kuogelea imeondoka jana kwenda Singapore kushiriki mashindano ya Dunia (World Aquatics Championship) yatakayofanyika kuanzia Julai 27 hadi Agosti 3, 2025. Waogeleaji walioteuliwa ni Collins Saliboko na Michael Joseph, ambao waliweka kambi ya maandalizi Afrika Kusini.

Collins atashindana kwenye mita 100 kwa mtindo wa Butterfly, huku Michael akishiriki mita 50 kwa mtindo huo huo. Mkurugenzi wa mashindano wa TSA, Amina Mfaume, amesema wachezaji wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanapunguza muda wao wa rekodi na kupeperusha bendera ya Tanzania.
Rais wa TSA, David Mwasyoge, amesema lengo ni kuona wanarudi na medali za ushindi, huku akieleza kuwa mafanikio yao yatafungua milango ya kushiriki Olimpiki ya Septemba. BMT kupitia kwa Ofisa wake wa habari, Charles Maguzu, imepongeza juhudi za TSA katika kukuza mchezo huo na kuwataka waogeleaji hao kufuata maelekezo ya walimu wao.