Thursday, March 12, 2026
spot_img
HomeHabariTume Vurugu Uchaguzi yajadiliwa Geneva

Tume Vurugu Uchaguzi yajadiliwa Geneva

Tanzania imeeleza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha uwajibikaji, maridhiano na kuendelea kuzijenga taasisi za umma kupitia kuundwa kwa Tume Huru ya Uchunguzi kuhusu vurugu, uharibifu wa mali na madai ya vifo vilivyohusishwa na Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025.

Hatua hiyo iliangaziwa katika tukio maalum lililofanyika sambamba na Kikao cha 61 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika mjini Geneva, Uswisi.

Katika uwasilishaji huo, Tume hiyo ilielezwa kuwa ni chombo muhimu cha kitaifa kilichoanzishwa kwa lengo la kuweka wazi ukweli kuhusu matukio hayo, kuimarisha imani ya umma na kusaidia juhudi za taifa katika kukuza uwajibikaji, maridhiano na utawala wa kidemokrasia.

Akizungumza katika tukio hilo,  Mkurugenzi Msaidizi wa Ufatiliaji wa Haki, Wizara ya Katiba na Sheria, Beatrice Mpembo alisema Tume hiyo iliundwa na Rais Samia tarehe 18 Novemba 2025 kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, kwa lengo la kuchunguza matukio hayo na kuishauri Serikali kuhusu hatua stahiki zinazopaswa kuchukuliwa.

Alieleza kuwa Tume hiyo ni chombo huru, maalum na cha muda cha uchunguzi na usimamizi wa ukweli, chenye jukumu la kuchunguza chanzo cha vurugu hizo, kupitia matukio yaliyofuata baada yake pamoja na kutathmini hatua zilizochukuliwa katika kipindi hicho. Lengo kuu ni kuimarisha uwajibikaji na kusaidia kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi na mifumo ya kitaifa.

Tume hiyo inaongozwa na Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania na mtaalamu wa sheria anayeheshimika kwa mchango wake katika uadilifu wa mifumo ya sheria, haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya jinai. Anasaidiwa na makamishna wengine wanane, wakiwemo wanawake wawili na wanaume sita wenye uzoefu katika maeneo ya utawala bora, sheria na utulivu, usalama, maendeleo na utawala.

Kwa mujibu wa uwasilishaji huo, Tume imepewa jukumu la kuchunguza visababishi vya msingi vya vurugu hizo, ikiwemo malalamiko ya vijana na nafasi ya vitendo vya upinzani; kutathmini hatua zilizochukuliwa na vyombo vya usalama katika kurejesha utulivu; pamoja na kupendekeza hatua za kuimarisha maridhiano na mshikamano wa kijamii.

Majukumu mengine ni pamoja na kuchunguza uwezekano wa ufadhili kwa waliohusika katika vurugu hizo na kupendekeza mageuzi yatakayosaidia kuzuia vurugu za uchaguzi zijazo na kuimarisha taasisi za kidemokrasia.

Tanzania pia ilisisitiza kuwa uwazi na ushiriki wa wananchi ni msingi muhimu wa utekelezaji wa kazi za Tume hiyo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tovuti ya umma iliwekwa ili kutoa taarifa kuhusu muundo wa Tume, hadidu za rejea na njia ambazo wananchi wanaweza kutumia kushiriki katika mchakato huo kupitia barua, simu na mitandao ya kijamii.

Aidha, Tume ilifanya mkutano na vyombo vya habari ulioonyeshwa kitaifa tarehe 1 Desemba 2025 uliowakutanisha wahariri na wawakilishi wa vyombo vya habari, kabla ya kuendesha vikao vya hadhara na vya faragha vilivyowahusisha mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, watumishi waandamizi wa umma, wananchi, wasomi na wawakilishi wa asasi za kiraia.

Kwa mujibu wa uwasilishaji huo, matokeo ya Tume yanatarajiwa kusaidia si tu katika uwajibikaji bali pia katika maridhiano mapana ya kitaifa na mageuzi ya muda mrefu.

Kutokana na hilo, Serikali imependekeza kuanzishwa kwa Mpango wa Kitaifa wa Maridhiano utakaolenga kurejesha amani na utulivu, kuponya mipasuko ya kijamii, kuhimiza ukweli na majadiliano, kushughulikia malalamiko ya kihistoria na kuzuia migogoro ya baadaye.

Hatua nyingine zilizotajwa kuwa zimechukuliwa na Serikali baada ya uchaguzi ni pamoja na kutoa msamaha kwa vijana 1,787 waliobainika kuwa na makosa madogo yaliyohusiana na matukio hayo, pamoja na kuanzishwa kwa wizara mpya ya vijana chini ya Ofisi ya Rais iliyotangazwa tarehe 17 Novemba 2025 kwa lengo la kushughulikia changamoto za ajira, maendeleo ya ujuzi na ushiriki wa vijana katika maendeleo ya taifa.

Awali Tume hiyo ilipewa muda wa siku 90 kukamilisha kazi yake, lakini baadaye iliongezewa siku 42 kutokana na mwitikio mkubwa wa umma, na inatarajiwa kuwasilisha taarifa yake mwezi Aprili 2026.

Tanzania imesema kuwa Tume hiyo inaakisi dhamira ya nchi katika kuimarisha haki, uwajibikaji, haki za binadamu na utawala shirikishi, huku ikiweka msingi wa amani endelevu, taasisi imara na mshikamano wa taifa wa muda mrefu.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments