TVLA yagusa mioyo ya wafugaji maonesho ya Nanenane

Na Daudi Nyingo, Dodoma

Katika kuadhimisha Maonesho ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Nzuguni, mkoani Dodoma, Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) umeendelea kugusa mioyo ya Wafugaji kwa kutoa huduma na elimu inayolenga kuboresha afya ya mifugo nchini.

Akizungumza Leo Agosti 07, 2025  katika banda la TVLA, Meneja wa Kituo cha TVLA Dodoma, Dk. Japhet Nkangaga, amesema kuwa wakala inajihusisha na utoaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya mifugo, upimaji wa sampuli, utengenezaji wa chanjo, pamoja na tafiti za kisayansi zinazolenga kuboresha afya na uzalishaji wa mifugo nchini.

“Katika Maonesho haya ya Nanenane kwa nchi nzima, tumetoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa kabla ya matibabu, umuhimu wa kuchanja mifugo, na madhara ya kutumia dawa bila vipimo,”

“Hhadi kufikia siku ya saba ya maonesho, kwa upande wa Dodoma pekee TVLA tayari imehudumia zaidi ya wadau wa mifugo zaidi ya 800 waliotembelea banda letu, wengi wao wakionyesha kiu ya maarifa na kuomba ushauri kuhusu magonjwa yanayoathiri mifugo yao.” ameeleza Dk. Nkangaga.

Dk. Nkangaga ametoatoa wito kwa wafugaji wote nchini kuwatumia wataalamu wa mifugo na vituo vya uchunguzi kama TVLA kwa ajili ya vipimo sahihi vinavyopatikana katika maabara za TVLA kanda zote kuchunguza na kutambua  magonjwa yanayowapata wanyama, kutumia chanjo kukinga wanyama dhidi ya magonjwa kwa kutumia chanjo bora TVLA pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu.

Gaudensia Simwanza, mfugaji kutoka Chamwino, amesema kuwa amejifunza mambo mapya kuhusu njia sahihi za kutibu mifugo yake kwani kabla hajapata elimu alikuwa anatibu mifugo yake kwa mazoea na mara nyingi bila vipimo, lakini baada ya kupata maelezo kutoka kwa wataalamu wa TVLA, amegundua kuwa hilo linaweza kuwa chanzo cha usugu wa dawa na kifo kwa mifugo.

Naye Frank Mvungi, mfugaji kutoka Kongwa, amesema elimu aliyoipata kuhusu chanjo kwa mifugo ambayo inaonekana haina dalili za ugonjwa imemfungua macho kwani alikuwa anadhani kwamba anatakiwa kuchanja mifugo ikianza kuumwa, kumbe chanjo ni kinga na ameahidi kuwashauri wenzake wachanje mifugo yao kabla ya kushambuliwa na magonjwa.

Maonesho ya Nanenane mwaka huu yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi kama TVLA kuwasogezea wafugaji elimu ya kisayansi na huduma bora kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya mifugo nchini.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *