Friday, February 20, 2026
spot_img
HomeHabariTVLA yatoa elimu ya matumizi sahihi ya chanjo za mifugo kwa wauzaji...

TVLA yatoa elimu ya matumizi sahihi ya chanjo za mifugo kwa wauzaji wa pembejeo Singida

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imeendelea kuimarisha juhudi za kulinda afya ya mifugo nchini kwa kutoa elimu kwa wauzaji wa pembejeo za mifugo mkoani Singida kuhusu utoaji na matumizi sahihi ya chanjo za mifugo zinazozalishwa na taasisi hiyo.

Zoezi hilo lililofanyika tarehe 19 na 20 Februari 2026 lililenga kuwajengea uwezo wauzaji wa pembejeo kama kiungo muhimu cha kuwafikia wafugaji, ili waweze kutoa elimu sahihi kuhusu utambuzi wa chanjo za TVLA, namna bora ya kuzitunza, matumizi sahihi na umuhimu wa kufuata taratibu za kitaalamu katika utoaji wa chanjo.

‎Akizungumza wakati wa kuhitimisha zoezi hilo tarehe 20 Februari 2026, Meneja wa TVLA Kanda ya Kati Dodoma, Dk. Japhet Nkangaga, alisema kuwa ziara hiyo ililenga kutoa elimu kwa wauzaji wa pembejeo na wafugaji kuhusu matumizi sahihi ya chanjo ya Matone (TEMEVAC), ikiwemo namna bora ya kuzipokea, kuzihifadhi katika ubaridi unaostahili ili kudumisha ubora wake na kuhakikisha chanjo zinatumika kwa ufanisi unaokusudiwa.

“Tunasisitiza matumizi sahihi kuanzia hatua ya kufungua chupa ya chanjo. Kama imeandikwa kuwa na dozi 100, ni lazima itoe dozi 100. Endapo tundu litatobolewa kubwa, kunakuwa na uwezekano wa chanjo kutoka nyingi zaidi na kusababisha dozi zilizokusudiwa kutotimia,” alisema Dk. Nkangaga.

‎Aliongeza kuwa elimu hiyo pia inahusisha matumizi sahihi ya chanjo baada ya kufunguliwa, akieleza kuwa kuku mmoja hupatiwa tone moja la chanjo na kurudiwa kuchanjwa baada ya miezi mitatu, utaratibu unaoendelea kwa mwaka mzima hadi kuku anapofikia hatua ya matumizi ya binadamu.

‎Baadhi ya wauzaji wa pembejeo za mifugo mkoani Singida wameibua changamoto ya upatikanaji wa chanjo mbalimbali, hali ambayo imekuwa ikiwalazimu wakati mwingine kupata chanjo kutoka vyanzo visivyo na uhakika.

‎Wameshauri TVLA kuimarisha upatikanaji wa chanjo ili kuhakikisha wauzaji na wafugaji wanapata bidhaa salama, zenye ubora na kutoka katika vyanzo vinavyoaminika, hatua itakayosaidia kudhibiti tatizo la chanjo zisizo halali sokoni.

‎Ester Munuo, muuzaji wa pembejeo za mifugo mkoani humo, alisema kuwa pamoja na chanjo ya Newcastle (TEMEVAC), kuna umuhimu wa TVLA kuongeza uzalishaji wa aina nyingine za chanjo za kuku, zikiwemo chanjo za gumboro na ndui, ili kuwapa wauzaji uhakika wa chanzo sahihi cha chanjo.

‎‎“Tunapopata chanjo kutoka mamlaka moja inayoaminika, inatusaidia kuepuka kuchukua chanjo kutoka vyanzo visivyo na uhakika, jambo ambalo linaweza kuleta changamoto kwa mtumiaji na kuathiri imani ya wafugaji,”alisema.

‎‎Kwa upande wake, Anthony Ntobi alisema kuwa upatikanaji wa chanjo kwa wakati na kupitia mamlaka rasmi utarahisisha kazi ya wauzaji na kuongeza ufanisi kwa wafugaji.

‎“Kuna baadhi ya chanjo za kuku ambazo wakati mwingine husambazwa kwa nyakati tofauti. Kupata chanjo moja kwa moja kutoka mamlaka husika kutarahisisha upatikanaji, kupunguza hatari ya chanjo feki na kutuwezesha kuwahudumia wafugaji kwa ufanisi zaidi,” alisema.

‎TVLA imeeleza kuwa itaendelea kutoa elimu kwa umma na wadau wa sekta ya mifugo katika mikoa mbalimbali nchini kama sehemu ya mkakati endelevu wa kitaifa wa kuimarisha afya za mifugo, kuongeza uzalishaji na kuchangia maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.


RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments