Uchunguzi wa Wafanyabiashara wa kigeni Kariakoo wafikia asilimia 50

📌…Yaaendelea kuwahoji wafanyabiashara

Kamati maalum iliyoundwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, kuchunguza uwepo wa wafanyabiashara wa kigeni katika eneo la Kariakoo imefikia asilimia 50 ya kazi yake na imeahidi kukamilisha ripoti hiyo ifikapo Machi 2, 2025, kama ilivyoagizwa.

Kamati hiyo yenye wajumbe 15 inaongozwa na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda Lwoga. Iliundwa Februari 2, 2025, kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Januari 30, 2025, wakati wa hafla ya chakula cha mchana kwa washiriki wa uokoaji wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la Kariakoo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki, Profesa Lwoga alieleza kuwa mara baada ya kuteuliwa, kamati ilianza kazi kwa kuwahoji wafanyabiashara wa makundi mbalimbali, wakiwemo machinga, wauza vifaa vya umeme, vipodozi, vifaa vya magari na wafanyabiashara wengine.

“Hata leo tupo na wafanyabiashara wa Kariakoo tukizidi kupata taarifa zaidi kuhusu changamoto ya uwepo wa wafanyabiashara wa kigeni ili tuweze kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kuondoa changamoto hii,” alisema Profesa Lwoga.

Aliongeza kuwa kamati imeweka namba ya simu ya bure kwa wananchi wote kutoa maoni yao, ambapo wanaweza kupiga 080011616 au kutuma ujumbe kupitia WhatsApp kwa namba 0738 816113.

Mjumbe wa kamati hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Conrad Millinga, alieleza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha biashara zinazofanyika nchini zinawanufaisha zaidi Watanzania huku wageni wakiheshimu sheria za biashara za Tanzania.

“Hatupingi wageni kufanya biashara hapa nchini, lakini wanapaswa kuendesha shughuli zao kwa kufuata taratibu zilizopo, si kufanya holela,” alisema Millinga.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severini Mushi, aliwasihi wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo kwa kutoa maoni yao, akisisitiza kuwa ushirikiano mzuri utaharakisha utatuzi wa changamoto hiyo.

Kwa upande wake, Mjumbe wa kamati kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ted Sikuluwasha, alisema kuwa kamati hiyo pia inafanya mahojiano na baadhi ya taasisi za serikali ili kupata suluhisho bora kwa changamoto hiyo na kuhakikisha ushindani wa biashara unakuwa sawa kati ya wageni na Watanzania.

“Tutahakikisha ripoti yetu inakuwa na mapendekezo yenye kuleta suluhisho la kudumu kwa changamoto hii, na tunajitahidi kukamilisha kazi kwa wakati,” alisema Sikuluwasha.

Kamati hiyo imeahidi kuwasilisha ripoti yake kwa Waziri wa Viwanda na Biashara ifikapo Machi 2, 2025.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *