Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa meli nne za mizigo katika Bandari ya Karema mkoani Katavi unatajwa kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mikoa ya Magharibi mwa Tanzania na nchi jirani zinazotumia Ziwa Tanganyika.
Pia kunatarajiwa kufungua fursa za kiuchumi ikiwemo kuongezeka kwa biashara za ndani na kimataifa, ajira kwa wananchi na kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.
Msimamizi Msaidizi wa Bandari ya Karema, Anthony Poyo aliyasema hayo juzi wakati wa tukio la kuingizwa majini kwa meli ya nne baada ya kukamilika kuundwa, kwamba kila meli ikiwa na uwezo wa kubeba tani 2,000 za mizigo.
Poyo alisema kukamilika kwa meli hizo kutaimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia.




Alisema kupitia meli hizo, mizigo mbalimbali ikiwemo mazao ya kilimo, madini na bidhaa nyingine zitasafirishwa kwa urahisi kupitia Ziwa Tanganyika kwenda bandari nyingine na hatimaye kufika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Poyo alisema mradi huo unatarajiwa pia kuongeza ajira kwa wananchi wa maeneo ya Karema na mikoa ya jirani kupitia shughuli za usafirishaji, upakiaji wa mizigo, huduma bandarini pamoja na biashara ndogo ndogo zitakazozunguka bandari hiyo.
“Ujenzi wa meli hizi kumetokana na serikali kufungua fursa ya uwekezaji. Sisi kama TPA itatuongezea kupata mizigo mingi. Meli moja inamita 70, ukubwa wa gati ni mita 150. Itaongeza uchumi wa Taifa na mtu mmoja mmoja,” alisema Poyo na kuongeza;
“Hivi sasa tuna reli ya SGR, wamiliki wa malori watanufaika kwa kuchukua mizigo katika bandari hii. Tani 10,000 za mizigo tunahudumia katika bandari hii, hivyo kuja kwa meli hizi kutaongeza hadi tani 8,000 kwa wakati mmoja”
Poyo alisema ujio wa meli hizo kutawezesha kubeba madini aina ya lithium, dhahabu, shaba na nickel kutoka DRC kuja hapa nchini na kusafirishwa kwenda Ulaya.
Kwa upande wa wakulima na wafanyabiashara, Poyo alisema utarahisisha usafirishaji wa mazao kwenda katika masoko makubwa ya kikanda na kimataifa, kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko na kuongeza kipato cha wananchi wa Mkoa wa Katavi na maeneo jirani.
Meneja Rasilimali Watu kutoka Kampuni ya Ankola Shipyard Co.Ltd ambao ndiyo waliounda meli hizo, Mohammed Chande alisema ujenzi wa meli hizo ulianza Aprili mwaka jana na ukitarajiwa kukamilika Julai 2026. Mpaka sasa umefikia zaidi ya asilimia 95, huku meli zote zikiwa majini kwa hatua mbalimbali za uhakiki wa mwisho kuanza kutoa huduma.


“Kukamilika kwa meli hizi kutafungua njia na mlango wa kiuchumi Ziwa Tanganyika. Utaleta fursa nchini hususani kwa vijana. Tangu mradi ulipoanza vijana wengi wamepata ajira,” alisema Chande.
Chande alisema siri ya kuwahi kumalizika mapema kwa mradi huo ni mazingira mazuri ya kufanya kazi Tanzania ikiwamo ushirikiano na serikali.
Kuhusu changamoto, Chande alisema wakati wa utekelezaji walikumbana na mabadiliko ya hali ya hewa kama vile upepo mkali mkali na mvua kubwa kunyesha.
Baadhi ya wavuvi katika Ziwa Tanganyika akiwamo Joseph Raphael alisema: “Hizi meli zitaleta fursa kwetu vijana kwa sababu zitatuwezesha kupata ajira.Tutaweza kupakia mizigo”.
Mei 12 mwaka jana Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alifanya ziara katika Bandari ya Karema kuangalia ujenzi wa meli hizo.
Akiwa bandarini hapo alisema zikikamilika zitainufaisha Tanzania kwani usafirishaji wa shehena ya mizigo kutoka Bandari ya Kigoma unategemea kutumia miundombinu ya reli ya MGR na SGR hadi Bandari ya Dar es Salaam na Tanga.
Pia alisema kazi kubwa ambayo serikali inaifanya ni kuhakikisha inaboresha bandari, miundombinu ya reli ya kati na ile ya SGR na jengo la abiria kwenye Uwanja wa Ndege Kigoma, ili sekta ya usafirishaji iwe bora na isiwe kikwazo kwa wananchi na wawekezaji.
Kihenzile alisema reli ya kati kutoka Tabora – Mpanda hadi Karema ikikamilika itarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini hapo hadi Dar es Salaam.





