Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, amepongeza taasisi za Umma kwa kupiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma kwa umma kwani yameongeza ufanisi.

Mhandisi Zena ameyasema hayo Julai 23, 2025 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Maafisa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala (TAPA-HR) katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa, AICC jijini Arusha.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni ‘Mwelekeo mpya wa nafasi ya wataalamu wa usimamizi wa rasilimali watu na utawala kusukuma mabadiliko kuendana na mageuzi ya teknolojia’.
“Wakati natembelea mabanda ya Maonesho hapo nje, nimeelezwa kila nilipoenda jinsi matumizi ya huduma mtandao yalivyoongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi hili ni jambo zuri.” amesema.
Kabla ya kufungua mkutano huo, Mhandisi Zena ametembelea mabanda ya Maonesho likiwemo banda la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ambapo Afisa Uhusiano wa PSSSF, Aisa Kimaro, alimueleza Mhandisi Zena kuwa kwa zaidi ya asilimia 95, huduma za PSSSF zinatolewa kwa njia ya mtandao (PSSSF Kidijitali) hali ambayo imeongeza ufanisi katika utoaji huduma.





