KUELEKEA kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo yatafanyika Machi 8 mwaka huu mkoani Arusha na kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wanawake zaidi ya 150 wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Kanda ya Kaskazini, wamezindua wiki ya maadhimisho hayo, kwa kutembelea leo vivutio vya Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.

Wanawake hao waliingiza katika Ziwa Manyara kwa nderemo na vivijo kwa kucheza ngoma pamoja na kufungua shampain kwenye lango kuu la kuingia hifadhi hiyo na kuvuta watalii wanawake waliokuwa wakitoka Hifadhi ya Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro kushindwa kujizuia kuendelea na safari zai na kusimamisha magari yao na kuungana pamoja kucheza.
Akizungumza leo katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara,wakati akiongoza msafala wa wanawake hao, Naibu Kamishna wa Uhifadhi ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini TANAPA,Steria Ndaga amesema wanawake hao ni wafanyakazi wa TANAPA makao makuu, hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Momela,Tarangile Ziwa Manyara na Mkomanzi.
Amesema wamezindua wiki ya siku ya wanawake duniani, ambayo maadhimisho yake Machi 8 mwaka huu kwa kutembelea hifadhi hiyo, ambayo wameitumia kama fursa muhimu ya kutambua mchango wa wanawake katika ulinzi wa uhifadhi wa maliasili na wanyamapori nchini.

“Tumejipanga wanawake sisi wa TANAPA katika wiki hii kwa kufanya shughuli mbalimbali kuanzia Machi Mosi hadi kilele Machi 8 na kutakua na shughuli nyingi ikiwemo Machi 4 kupata masomo toka kwa wataalamu mbalimbali ya kuboresha akili zetu, ili kuleta mafanikio zaidi kwenye utendaji kazi wetu na familia zetu lakini, tutatembelea pia wenye mahitaji maalumu na kula nao na kushinda nao,”amesema
Amesema pia wataungana na Mkuu wa Mkoa Arusha Paul Makonda, kwa kufanya shughuli mbalimbali zilizopangwa kufanyika.
Aidha amesema walianza utalii wao katika lango kuu la kuingia hifadhi ya Ziwa Manyara na kufanya utalii wa kutembea kwa kamba juu,kupanda boti ndani ya Ziwa Manyara na kuona vivutio vya maporomoko ya maji ya Mto Endabash.
“Kila mwaka tutahakikisha tunafanya matukio haya kulingana na ratiba zetu na haya yote tunaunga mkono juhudi za Rais Samia Hassan Suluhu ambaye ni mhifadhi namba moja nchini, kwa jitihada zake za kutangaza utalii duniani sasa tunaona watalii wanafurika kwenye hifadhi zetu.


“Mwaka huu msimu wa utalii ukianza tunatarajia kupata wageni wengi zaidi na hivyo tunaendelea kuwasihi wadau wa utalii kuendelea kuwekeza kwenye kuongeza miundombinu ya malazi na mengine ili wageni hao wapate huduma zote muhimu wafikapo nchini,”amesmea.
Amemshukuru Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, kwa kuwaruhusu wanawake kutumia siku 8 kusherehekea siku ya wanawake duniani, tofauti na waajiri wengine.
Amewahimiza kuendelea kujenga mazingira ya kupendana yanayoweza kushirikisha wanawake wenzao, ndio sababu iliyowasukuma wao kuungana watumishi wa TANAPA na familia zao ili kuvuta walioko nyuma kwenye utalii kuamka na kuwa mstari wa mbele.


Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dk Yustina Kiwango, ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara,amesema wamezindua wiki ya maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani kwa kutembelea vivutio mbalimbali kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara ikiwa ni kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kutangaza maliasili mbalimba nchini.
“Tunahimiza kulinda na kuhifadhi maliasili hasa za wanyamapori nchini, lakini tunaelewa rasilimali za wanayamapori zinatuletea watalii kwa wingi na utalii huu unachangia pato la taifa takribani asilimia 21 za fedha za kigeni nchini, hii hii sio fedha ndogo nanhili ndilo linatupa nguvu kuendelea kulinda na kutangaza,kulinda rasilimali zetu,”amesema.

Ameomba wanawake nchini kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi za taifa kama Ziwa Manyara kujionea vivutio vya maporomoko ya maji ya Mto Endabash m, Ziwa Manyara lenyewe ambalo unaweza kufanya utalii wa kupiga kasia, kufanya utalii kwa kutembea juu ya miti ambalo ni zoezi zuri na la kusisimua.


