Waogeleaji wa Tanzania, Collins Saliboko na Michael Joseph, wanatarajiwa kuondoka nchini Julai 24 kuelekea Singapore kushiriki mashindano ya Dunia yatakayofanyika kuanzia Julai 27 hadi Agosti 3.

Mkurugenzi wa Mashindano wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Amina Mfaume, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na wachezaji hao wako kambini Afrika Kusini kwa maandalizi ya mwisho.
“Wanafanya mazoezi ya kuimarisha pumzi na wanajituma sana. Tuna imani watafanya vizuri kwa kupunguza muda wao wa kuogelea,” alisema Mfaume.
Wataongozwa na Kocha Mkuu John Mbelea, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa TSA.
Kwa upande wake, Saliboko alisema: “Najua kutakuwa na ushindani mkubwa lakini tuna lengo moja – kuipeperusha bendera ya Tanzania kwa heshima. Tunaomba Watanzania watuombee.”