Saturday, October 11, 2025
spot_img
HomeBiasharaWauzaji wa chanjo wafikiwa na TVLA

Wauzaji wa chanjo wafikiwa na TVLA

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imeendelea na ufuatiliaji wa huduma zake kwa wateja kwa kutembelea wauzaji wa bidhaa zake, hususan chanjo za mifugo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja inayoendelea kote nchini.

Lengo ni kubaini namna huduma za TVLA zinavyowafikia wateja, kusikiliza maoni ya wadau wanaosambaza bidhaa hizo, pamoja na kujadili njia bora za kuimarisha ubora na upatikanaji wa huduma.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika tarehe 10 na 11 Oktoba 2025 katika mikoa ya Tabora na Shinyanga, Afisa Habari wa TVLA – Dar es Salaam, Daudi Nyingo, alisema kuwa TVLA inalenga kuimarisha uhusiano wake na wadau wa sekta ya mifugo na kuhakikisha bidhaa zake zinaendelea kukidhi mahitaji halisi ya wafugaji nchini.

“Tumekuja kuwasikiliza ili kufahamu changamoto mnazozipata kutoka kwenu wenyewe pamoja na wafugaji mnaowauzia bidhaa zetu (chanjo).

Tunataka kuhakikisha kila mteja wa TVLA anapata huduma bora, bidhaa zenye ubora, na taarifa sahihi. Ushirikiano wenu ni msingi wa maboresho tunayoyafanya kila siku,”alisema Nyingo.

Kwa upande wake, Meneja wa TVLA Kanda ya Magharibi, Dk. Qwari Bura, alibainisha kuwa TVLA imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa zake kwa wakati na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya chanjo kwa wadau wote, kwani kila mfugaji na kila duka linalouza bidhaa za TVLA linapaswa kuwa na taarifa sahihi kuhusu bidhaa na jinsi ya kuzitumia ipasavyo.

Wauzaji wa bidhaa za TVLA katika mikoa hiyo walipongeza hatua ya maafisa hao kufika kwao moja kwa moja, wakisema ni mfano bora wa taasisi ya umma inayowajali wateja wake.

Rosemary Renatus wa Tabora alisema kuwa TVLA imekuwa ikitoa bidhaa bora, lakini wanashauri kuimarishwa zaidi kwa mawasiliano na taarifa za bidhaa mpya. Ziara kama hizi zinawapa nafasi ya kueleza changamoto zao moja kwa moja.

Naye Abel Kalenzo kutoka Shinyanga alisema hatua hiyo imeongeza imani kwa wateja na imeonesha uwajibikaji wa taasisi hiyo kwa wadau wa sekta ya mifugo.

Ziara hizo ni mwendelezo wa kampeni ya TVLA katika Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka 2025, inayolenga kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya mifugo, kuongeza ufanisi wa mawasiliano, na kuboresha huduma katika ngazi zote za taasisi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments