Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu),Ridhiwani Kikwete, amesema kuwa Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro (KLICL) kipo katika hatua nzuri ya uzalishaji na kinaendelea kuimarika.

Akizungumza leo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Serikali (PIC) katika kiwanda hicho kilichopo mjini Moshi, Waziri Kikwete alisisitiza umuhimu wa kufanikisha malengo ya kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa ubia kati ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Jeshi la Magereza.
“Jukumu langu kubwa ni kuhakikisha kuwa mipango na malengo tuliyojiwekea yanafikiwa. Niwahakikishie kuwa, mara kiwanda hiki kitakapofikia uzalishaji wa asilimia 100, kitazalisha faida kubwa, kupunguza gharama, na kuimarisha sekta ya ngozi nchini,” alisema Waziri Kikwete.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru, alieleza kuwa mfuko huo una mkakati wa kuwekeza katika miradi mbalimbali yenye manufaa kwa jamii, ikiwa ni sehemu ya dhamira yao ya kukuza uchumi na ajira.




Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Mhe. Augustine Vumma Hole, aliishauri menejimenti ya kiwanda hicho kuboresha bidhaa zao ili kuendana na mahitaji ya soko la sasa bila kuacha ubora wa kitaifa na kimataifa.
“Jitahidini sana kufuata mwelekeo wa fasheni bila kupunguza ubora wa bidhaa zenu. Mpaka sasa mmefanya kazi nzuri, lakini ongezeni ubunifu zaidi ili kufanikisha ushindani wa kimataifa,” alisema Mhe. Vumma.
Aidha, wajumbe wa kamati hiyo walipongeza jitihada za kiwanda hicho na kushauri kufanyika kwa juhudi zaidi za kutafuta ushirikiano na kampuni kubwa za kimataifa zinazozalisha bidhaa za ngozi ili kupanua soko na kuongeza tija kwa kiwanda.


