Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amesema kuwa hatua ya Halmashauri ya Tunduma kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 4.6 kwa vikundi 150 ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Mikopo hiyo, inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, imelenga vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa mfumo mpya wa utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo.
Akizungumza leo, Februari 25, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Songwe, Waziri Kikwete alieleza kuwa Rais Samia alielekeza kupitia na kuboresha utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo ili kuhakikisha inaleta tija kwa walengwa.
Baada ya maboresho hayo kukamilika, dirisha la utoaji wa mikopo lilifunguliwa rasmi mnamo Septemba 2024.
Aidha, Waziri Kikwete amepongeza juhudi za Rais Samia katika kuwawezesha vijana kwa kuwapatia fursa mbalimbali za kiuchumi.




Alisisitiza kuwa maelekezo ya Rais yanaendelea kutekelezwa kwa vitendo na Halmashauri pamoja na Serikali Kuu, huku akivitaka vikundi vilivyonufaika kutumia fedha hizo kwa miradi yenye tija na kurejesha mikopo kwa wakati ili wengine waweze kufaidika.
Katika hatua nyingine, Waziri Kikwete alikagua na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi kadhaa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa majengo ya Hospitali ya Halmashauri ya Momba, jengo la NMB, majengo ya madarasa ya ghorofa katika Shule ya Sekondari Uwanjani, pamoja na kikundi cha vijana cha ufugaji wa kuku Chipaka.




Waziri huyo pia aliwapongeza Wabunge wa majimbo ya Momba na Tunduma, Condester Sichwale (Momba) na David Silinde (Tunduma), kwa kuhakikisha wanatafsiri kwa vitendo maono ya Mhe. Rais Samia kwa kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika mkoa huo. Alibainisha kuwa miradi hiyo inachochea mapato ambayo husaidia Halmashauri za mkoa huo kuimarika kiuchumi na kuwezesha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani.