Yanga yampigia hesabu Feitoto kwa mkakati mzito wa usajili

Klabu ya Yanga SC ipo kwenye nafasi nzuri ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Feitoto’, ambaye amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake.

Yanga imetajwa kuwa imetoa ofa nono ya Sh milioni 750 kwa mkataba wa miaka miwili, sambamba na mshahara wa Sh milioni 40 kwa mwezi.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema Yanga imejipanga kumchukua Feitoto kama mbadala wa Stephane Aziz Ki, ambaye anahusishwa na kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco mwishoni mwa msimu huu. Kwa sasa, Yanga imewaacha mbali wapinzani wao Simba waliotoa ofa ya Sh milioni 600 kwa nyota huyo wa Zanzibar.

Hata hivyo, Azam FC bado inammiliki mchezaji huyo na inafanya jitihada za kumbakiza kwa kumpa mkataba mpya wenye maslahi bora zaidi. Pia, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini nayo inatajwa kuwa na nia ya kumsajili Feitoto, jambo linaloonyesha ushindani mkubwa wa kumnasa kiungo huyo.

Feitoto alitokea JKU ya Zanzibar na kufika Singida United kabla ya kutua Yanga mwaka 2018, kisha kujiunga na Azam FC mwaka 2023. Kwa sasa hajatia saini popote, lakini jina lake limekuwa gumzo kubwa kuelekea dirisha lijalo la usajili baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu huu.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *