Yanga yaonyesha ubabe, yaichapa Tabora United 3-0

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wameonyesha ubabe wao kwa kuichapa Tabora United mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora. Ushindi huo umeiwezesha Yanga kulipa kisasi cha kufungwa 3-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Israel Mwenda, Clement Mzize, na Prince Dube, huku ushindi huo ukiifanya timu hiyo kufikisha pointi 61. Mzize na Dube sasa wana mabao 11 kila mmoja, wakimfuatia Jean Ahua wa Simba mwenye mabao 12.

Mchezo huo ulianza kwa kasi, Yanga ikitawala na kujaribu mashambulizi kadhaa kabla ya Mwenda kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 21 kwa mpira wa adhabu. Bao la pili lilifungwa na Mzize dakika ya 56 baada ya makosa ya safu ya ulinzi ya Tabora United. Dube alihitimisha ushindi huo kwa bao la tatu lililotokana na uzembe wa viungo wa Tabora.

Kwa matokeo hayo, Yanga inaendelea kuongoza ligi, huku Tabora United ikibaki na pointi 37 katika nafasi ya tano, ikihatarisha ndoto zao za kufuzu michuano ya kimataifa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *