Kocha Mkuu wa Timu ya Zimamoto, Mohamed Alhilal (Teddy), amesema kuwa timu yake imejipanga kuhakikisha inafika fainali ya Kombe la Muungano licha ya ushindani mkali uliopo.

Leo Aprili 25, Zimamoto itashuka dimbani kumenyana na Coastal Union ya Tanga katika uwanja wa Gombani saa kumi alasiri, huku usiku KMKM SC wakipambana na Azam FC.
Hilali amesema ameandaa kikosi chake kuondoa hofu kwa wachezaji kwa kuwa wanakutana na timu yenye uzoefu mkubwa kutoka Ligi Kuu. Ametumia muda wa mazoezi kuwajenga wachezaji kisaikolojia na kiufundi ili kuwa tayari kukabiliana na wapinzani.
Kocha huyo ameeleza kuwa wanaamini kila kitu kinawezekana ndani ya dakika 90 za mchezo wa mpira wa miguu, na lengo lao ni kupita hatua hii kuelekea kwenye fainali ya mashindano hayo. Pia amesema mashindano hayo ni fursa ya kipekee kwao kujiimarisha kuelekea ligi na Kombe la FA.
Zimamoto SC inatumia michuano hii kama jukwaa la kuonyesha ubora wa wachezaji wake na pia kujifunza mbinu mpya ambazo zitawasaidia kwenye mashindano yajayo. Mashabiki wa timu hiyo wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti.