Nyota wa kimataifa wa Togo, Samuel Asamoah (31), yupo katika hatari kubwa ya kupooza mwili mzima baada ya kupata ajali mbaya uwanjani wakati akiichezea timu yake Guangxi Pingguo kwenye ligi daraja la pili nchini China.
Ajali hiyo ilitokea katika mchezo dhidi ya Chongqing Tonglianglong uliofanyika Jumapili iliyopita, ambapo Asamoah aligongana na mchezaji wa timu pinzani, Zhang Zhixiong, kabla ya kujigonga kwa nguvu kwenye bango la matangazo lililoko kando ya uwanja.
Video ya tukio hilo inaonyesha Asamoah akianguka chini bila kusogea, jambo lililolazimu madaktari wa timu kuingia haraka kumpa huduma ya kwanza.
Siku moja baada ya ajali, klabu yake ilitoa taarifa ikieleza kuwa mchezaji huyo amevunjika mifupa kadhaa ya shingo na kuathiri mishipa ya fahamu, hali inayomuweka katika hatari ya kupooza kabisa.
Klabu ilisema Asamoah amefanyiwa upasuaji wa dharura, lakini hatacheza tena msimu huu — huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa kutoonekana tena uwanjani.
