Wizara ya Maliasili na Utalii imesema ushindi wa Tanzania kwenye tuzo za World Travele Award 2025 ikiwemo tuzo kubwa ya Utalii wa safari bora duniani ni uthibitisho kuwa nchi ina vivutio vya utalii vinavyokubalika kimataifa.
Akizungumza Desemba 8, 2025 mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, akitokea Bahrain, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Hassan Abbas amesema ushindi huo unaonesha kuwa dunia imeitambua Tanzania kama kitovu bora cha utalii wa safari.
“Kwa mwaka wa pili mfululizo tumeshinda tuzo kubwa zaidi ya utalii wa safari duniani. Hii ni sawa na tuzo za Oscars kwa filamu au Grammy kwa muziki,” amesema Dk. Abbas.

Dk. Abbas ameongeza kuwa kutokana na ushindi huo, nchi imepewa heshima ya kuwa mwenyeki wa tuzo za dunia za utalii mwaka 2026, ambapo wadau wakubwa wa sekta hiyo duniani watakusanyika nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania , Ephraim Mafuru, amewashukuru wadau wa utalii kwa kuipigia kura Tanzania, akisema ushindi huo umetokana na imani ya dunia kwa Serengeti na hifadhi nyingine.
“Tanzania imeshinda tuzo ya Hifadhi bora duniani kupitia Serengeti, pamoja na tuzo ya Utalii wa Safari Bora Duniani mafanikio haya yametokana na serikali kuboresha miundombinu ikiwemo barabara zaidi ya kilomita 2,800 ndani ya hifadhi na kuvifanya vivutio kufikika kwa urahisi,” amesema Mafuru.






