Wednesday, December 10, 2025
spot_img
HomeElimuWanafunzi zaidi ya 500 kunufaika na mradi wa mabadiliko ya tabianchi

Wanafunzi zaidi ya 500 kunufaika na mradi wa mabadiliko ya tabianchi

Zaidi ya wanafunzi 500 wa shule za msingi na sekondari kutoka Tanzania na Malawi wanatarajiwa kunufaika na mafunzo maalum ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha ustawi wa jamii na kuongeza usalama wa chakula kupitia mradi mpya wa Pathway to Resilience.

Mradi huu umeanzishwa na vijana wawili kutoka Afrika Mashariki—Michael Mshana wa Tanzania na Shalom Mughogho wa Malawi—ambao ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nanhua nchini Taiwan. Wamebuni mradi huo kwa kutambua changamoto zinazozikabili nchi zao, ikiwemo ukame, mabadiliko ya mifumo ya mvua na kupungua kwa uzalishaji wa chakula.

Mradi unatekelezwa kupitia ufadhili wa Higher Education Sprout Program ya Taiwan, inayolenga kuwawezesha wanafunzi kushiriki katika suluhu bunifu za changamoto za kijamii.

Kwa wiki mbili mfululizo, mradi umejikita kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi kuhusu afya, lishe bora, stadi za maisha, matumizi sahihi ya teknolojia, na mbinu za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Pia unahusisha walimu na wahadhiri ili kuongeza ushirikiano wa moja kwa moja katika shughuli za kijamii.

Akizungumza wakati wa ziara ya mafunzo, Mshana alisema wanafunzi wamepata uelewa mpana kuhusu lishe na afya ya akili, pamoja na namna ya kubuni suluhu za kimazingira.

“Lengo letu ni kuwajengea vijana uwezo wa kutambua nguvu zao, kujiamini na kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya katika jamii,” alisema.

Kwa upande wake, Mughogho alibainisha kuwa Afrika bado inaendelea kuathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi, hivyo kuwaandaa vijana mapema ni msingi wa kujenga mustakabali salama wa chakula.

“Tunahitaji kizazi kinachoweza kufikiri kimkakati na kuchukua hatua za kweli za kulinda mazingira,” alisema.

Nchini Tanzania, mradi umefika katika Shule ya Msingi Ngomeni, Shule ya Sekondari Kilimanjaro, Chuo cha Ualimu Mhonda na Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA).
Kwa upande wa Malawi, shule zinazoshiriki ni kutoka maeneo yenye changamoto za kimazingira kama Mbalame, Magwero, Chinkhuti na Chuzu.

Mradi wa Pathway to Resilience unatarajiwa kupanuka zaidi kwa ushirikiano na taasisi za elimu, mashirika ya kijamii na wadau wa maendeleo ili kuwafikia vijana wengi zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments