Wananchi wa maeneo mbalimbali nchini watanufaika na minara mipya ya mawasiliano iliyojengwa na Airtel katika mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro itakayoongeza kasi ya upatikanaji wa huduma kwa wateja.
Minara hiyo imejengwa katika Mikoa ya Morogoro Wilaya ya Gairo Kata ya Magoweko, na Kihonda VETA, kijiji cha Yespa pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro Kata ya Sanya Juu. Minara hii ya mawasiliano inatarajiwa kuwainua kijamii na kiuchumi kupitia upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya uhakika.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa Airtel Kanda ya Kilimanjaro, Faustine Mtui, alisema, uzinduzi huo ni sehemu ya mkakati wa Airtel wa kutanua wigo wa upatikanaji wa huduma bora na za uhakika za mawasiliano kwa watu wote nchini.
“Uzinduzi huu unaonyesha dhamira ya kampuni ya Airtel Tanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kupanua huduma za mawasiliano na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.”
Alisema zaidi ya vijana 300 wilayani Gairo tayari wananufaika na ajira za uwakala kupitia Airtel, huku matarajio yakiwa kuwa uwepo wa mnara huo utaongeza ajira na kuboresha huduma za kifedha na kibiashara katika kata hiyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Magoweko, Shabani Sajilo, alisema, “Wananchi walikuwa wakikumbana na changamoto ya muda mrefu ya kukosa mtandao wa kuaminika, jambo lililoharibu mwenendo wa shughuli zao za kiuchumi, biashara na mawasiliano ya dharura.”
Alieleza, “Ujio wa mnara huU umekuwa suluhisho la kilio cha muda mrefu na utasaidia kuongeza tija katika shughuli za wananchi.”
Baadhi ya wananchi walioshiriki uzinduzi huo walionesha furaha yao kwa hatua hiyo muhimu wakisema itasaidia kufungua fursa za kiuchumi.
Happy Sembwa, mkazi wa Magoweko alisema, “Kwa muda mrefu kutokana na kukosa mawasiliano, hali ilitufanya kushindwa kupata taarifa muhimu, kufanya miamala ya kifedha na hata kuwasiliana na ndugu wakati wa dharura. Huduma hii mpya itafungua milango ya biashara mtandaoni, masomo kwa wanafunzi na urahisi wa kupata taarifa za kijamii na kiserikali.”
Uzinduzi huu uliambatana na ofa maalum ya siku tatu kwa wakazi wanaotumia minara hii, ambapo Airtel iliwawezesha kupata dakika 50 za kupiga mitandao yote, MB 500 za intaneti pamoja na SMS 50 ikiwa ni sehemu ya shukrani kwa wananchi wa maeneo hayo.
Minara hii inatarajiwa kuboresha kwa kiwango kikubwa mwenendo wa mawasiliano, kuongeza usalama wa kijamii na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa Tanzania




