📌Wananchi 10,660 katika wilaya sita kunufaika
📌Milioni 477 kugharamia Mradi huo
📌Serikali imelipa asilimia 80 na Wananchi watalipa asilimia 20 ya bei ya ununuzi kwa kila jiko
Dodoma📍
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na kampuni ya LS Solutions, wameanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa kusambaza majiko banifu kwa Wananchi wa mkoa wa Dodoma.
Akizindua Mradi huo jana, Rose Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ametumia fursa hiyo, kumtambulisha (Mtoa huduma) kampuni hiyo ya LS Solutions na kutoa wito kwa Wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa kununua majiko hayo kwa bei ya shilingi 11,200 (Bei ya ruzuku) ambapo kwa bei ya awali, majiko yalipaswa kuuzwa shilingi 56,000.
Wilaya zitakazonufaika ni wilaya ya Kondoa; Bahi; Chemba; Chamwino; Kongwa na Mpwapwa ambapo kwa kuanzia Mtoa huduma, ataanza usambazaji katika Wilaya ya Kondoa.


Senyamule amesema majiko hayo ambayo ni ya kisasa yanayotumia kuni na mkaa kidogo ikilinganishwa na majiko mengine, yanauzwa kwa bei ya punguzo baada ya Serikali kulipia asilimia 80; hivyo Mwananchi atalipia asilimia 20 iliyobaki ambayo ni himilivu.
“Majiko haya yana ruzuku ya Serikali ambapo jiko hili lingeuzwa kwa shilingi 56,000 sasa hivi litauzwa kwa shilingi 11,200 kwa sababu Serikali kupitia Wizara ya Nishati (Wakala wa Nishati Vijijini – REA) imechangia asilimia 80 ya bei ya majiko hayo na Mwananchi anakwenda kuchangia asilimia 20 tu lakini anapata jiko jipya na la kisasa kabisa na kazi yake ni kwenda kulitumia tu,” amesema Senyamule.
Senyamule ameongeza kuwa mkoa wa Dodoma umepata mgao wa majiko 10,660 ambayo yataanza kuuzwa katika wilaya sita, isipokuwa wilaya ya Dodoma Jiji ambapo kila Wilaya itapata majiko 1,777.
Ametoa wito kwa Wananchi wa Mkoa wa Dodoma, kuchangamkia fursa hiyo ya kipekee kwa kufika mapema katika maeneo yatakapokuwa yakiuzwa majiko hayo, wakiwa na vitambulisho vya taifa (NIDA) ambapo kila Kaya itauziwa jiko moja.


Naye Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi, Emmanuel Yesaya, amesema usambazaji wa majiko banifu kwa mkoa wa Dodoma ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi mkubwa wa kusambaza majiko laki 2 (200,000) nchi nzima kwa njia ya ruzuku ambapo Dodoma imepata mgao wa majiko 10,000 yenye thamani ya shilingi milioni 477.
“Majiko haya yanatumia mkaa na kuni kwa kiwango cha ufanisi wa hali ya juu, yameboreshwa, hayatoi moshi, yanatunza joto na yana “warrant” ya miaka miwili; wakati huo huo, yanadumu kwa muda mrefu”, amekaririwa, Mhandisi, Yesaya.





