Shughuli za utalii zinazochagizwa kwa sasa na ujio wa makundi ya familia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, yamechochea ongezeko la mapato yake kwa asilimia sita, ikikusanya Sh. bilioni 49.2 kati ya Oktoba mosi hadi Desemba 14 mwaka huu.
Watalii hao kutokea mataifa mbalimbali duniani, wanathibitisha na kuifanya sekta hiyo kuendelea kuonekana bado ni imara katika uchangiaji wa pato la taifa.
Akizungumza leo (Disemba 18,2025) na Waandishi wa Habari katika lango kuu la NAABI, Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Fabian Manyonyi, amesema kabla ya ongezeko hilo,mwaka uliopita waliingiza takribani Sh. bilioni 46.6.
“Tulikuwa tukiingiza takribani shilingi bilioni 46.6 na tuikilinganisha na mwaka huu kwa kipindi chote kuanzia Oktoba mosi hadi Desemba 14, tumeshaingiza bilioni 49.2, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia sita.
Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu mapato, Manyonyi anasema, “Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, tunaingiza mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka. Tukiangalia takwimu za wageni kwa mwaka 2023/2024, Serengeti ilipokea wageni 430,219.
…Wakati mapato kwa mwaka 2023/2024 yalikuwa shilingi bilioni 210.913 na mwaka 2024/2025, tulipokea wageni zaidi ya 491,398, huku mapato yakiwa shilingi bilioni 266.813.”




Kwa mujibu wa Manyonyi, hali ya utalii katika Hifadhi hiyo ya Serengeti, imeendelea kuimarika na kuwa ya kuridhisha zaidi kutokana na mtiririko wa wageni wanaoendelea na shughuli zao za kutembelea hifadhi hiyo ya taifa.
“Kwa kipindi cha mwaka jana, kumekuwa na ongezeko la wageni kwa kipindi kama hiki, ambacho ni kikubwa sana na kinatia matumaini, tukilinganisha kwa kipindi cha mwaka jana,”ameeleza.
Aidha, Ofisa Uhifadhi Daraja la Kwanza, anayeshughulikia utalii, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Susan Tesha, amesema wakati huu wa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, wameendelea kupokea wageni mbalimbali, wageni wa ndani na wa nje, wanaokwenda kushuhudia matukio ya uhamaji wa nyumbu, ambao kwa kipindi hiki wanakuwa maeneo ya kusini, ukanda wa Ndutu.
Raia wa Ujerumani, Michael Schlittenberver, ameeleza namna alivyovutiwa kuitembelea hifadhi hiyo: “Tutakuwa hapa kwa siku 16 lakini ni pamoja na Zanzibar pia. Utulivu, usalama wa wageni na ukarimu wa Watanzania, ndio ulionifanya mimi kuja Tanzania na familia yangu kufurahia vivutio hivi.”
Aidha, raia wa Uingereza, Talvinaer Virdee, amesema ameguswa kuja kuona vivutio vya Serengeti, baada ya miaka 30 tangu kuzaliwa kwake, kwa kuwa alizaliwa Tanzania na akahamia Uingereza na wazazi wake, akiwa na umri wa miaka sita.
“Nimemleta binti yangu pamoja nami, na nina watoto wawili, ambao hawakuweza kusafiri, lakini bila shaka nitakuwa nikiwarudisha kuja kuona Serengeti. Labda mwaka ujao na dada zangu watakuja,”amesema Virdee.
Muongoza watalii na mmiliki wa Kampuni ya World Serengeti Quest, Fidelis Fabian, amesema kwa uzoefu wake wa miaka 20 sasa,alisema watalii wengi wanakuja na familia zao, kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka.






