Friday, December 19, 2025
spot_img
HomeBiasharaSita waibuka na zawadi droo kubwa kampeni ya Simbanking ya Benki ya...

Sita waibuka na zawadi droo kubwa kampeni ya Simbanking ya Benki ya CRDB

• Wapo wawili waliojishindia gari, wawili walioshinda simu ya kisasa aina ya iPhone 17 Promax na wawili waliopata ufadhili wa kulipiwa ada ya chuo kikuu.

Dar es Salaam.  Desemba 2025: Wateja sita wa Benki ya CRDB wameumaliza mwaka 2025 kwa kishindo baada ya kuibuka washindi wa zawadi za aina tofauti za droo kubwa ya Benki ni Simbanking.

Katika washindi hao waliotangazwa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Stephen Adili katika droo hiyo, yupo Deo Ferdinand Mlawa wa kutoka Mikocheni jijini Dar es Salaam aliyejinyakulia gari aina ya Toyota Harrier Anaconda na Desderius Magombola kutoka Meru mkoani Arusha alijishindia gari aina ya Toyota IST New Model.

Adili amesema magari hayo yote mawili yamekatiwa bima kubwa na yatajazwa mafuta ‘full tank’ kabla ya kukabidhiwa kwa washindi ambao watatakiwa kuyaendesha tu.

“Toyota Harrier Anaconda ndio zawadi yetu kubwa mwaka huu. Nampongeza sana kaka Deo Ferdinand Mlawa kwa ushindi huu uliotokana na matumizi makubwa ya huduma zetu za Simbanking,” amesema Adili.

Kuhusu gari aina ya Toyota IST New Model, Adili amesema ni la sita kutolewa kwani tangu mwaka huu uanze mshindi mmoja alikuwa anajishindia kila baada ya miezi miwili.

“Nampongeza pia Desderius Douglas Magombola kwa ushindi huu mkubwa alioupata tukielekea kuufunga mwaka 2025. Yeye anaungana na washindi wengine watano waliojishindia Toyota IST New Model katika kampeni hii ya mwaka mzima ya Benki ni Simbanking. Nawasihi wateja wetu kuendelea kutumia huduma za Simbanking kwani wanaweza kuiuka washindi wa zawadi yoyote kati ya nyingi tunazozitoa. Kampeni hii itaendelea tena mwakani,” amesema Adili.

Kwenye droo hii kubwa kwa mwaka huu 2025, wanafunzi wawili wameibuka washindi hivyo watapata ufadhili wa kulipiwa ada. Wanafunzi hao, mmoja anasoma Chuo cha Usafiri wa Majini (DMI), Happiness Justine Chacha, na mwingine anasoma Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) jijini Dar es Salaam, John Simon Soka. 

“Wanafunzi hawa wote wawili watalipiwa ada ya masomo yao katika vyuo wanavyosoma. Ushindi wa wanafunzi hawa unatoa hamasa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kutumia huduma zetu za Simbanking kwani nao wanaweza kuibuka washindi kama hivi,” amesema Adili. 

Licha ya wanafunzi hao watakaolipiwa ada katika muhula ujao wa masomo yao, wapo pia wanafunzi wengine wawili wa vyuo vikuu walioibuka washindi wa simu za kisasa aina ya iPhone 17 Promax ambao ni Maimartha Haji Seleman wa Keko jijini Dar es Salaam na Felix Geofrey Sembwana naye wa jijini Dar es Salaam.

“Tulikuwa na zawadi za aina tofauti mwaka huu. Droo ya leo ni ushahidi kwamba kwa kila mteja wetu, kulikuwa na zawadi inayomfaa. Tunapohitimisha kampeni ya Benki ni Simbanking tunajivunia zawadi kemkem tulizozitoa kwa washindi wetu huku tukijipanga kuendelea nayo mwakani. Kwa wateja ambao hawakubahatika mwaka huu, nawasihi waendelee kutumia huduma za Simbanking mwakani kwani bahati yaweza kuwa yao nao wakapata kitu,” ameeleza Adili.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments