Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro imethibitisha kuwa uchunguzi wa awali wa kitabibu haujabaini dalili zozote za ukatili, udhalilishaji wala tukio baya lililofanywa kwenye mwili wa marehemu Mwanahasan Hamis, mkazi wa Kijiji cha Lusanga, Kata ya Diongoya, Tarafa ya Turiani wilayani Mvomero.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya ndugu wa marehemu kutilia shaka kifo chake, hali iliyoibua vurugu Januari 17 mwaka huu, zilizohusisha kuchomwa moto kwa magari mawili yaliyokuwa yakitumika kusafirisha waombolezaji, pamoja na kusababisha majeruhi kwa baadhi ya wananchi.
Mwanahasan Hamis alikuwa mfanyakazi wa majumbani katika nyumba ya Miraji Chomoka jijini Dar es Salaam, na kifo chake kilizua taharuki baada ya baadhi ya ndugu na wananchi kudai kuwepo kwa dosari kwenye mwili wake.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi liliingilia kati na kuuchukua mwili wa marehemu na kuufikisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya uchunguzi wa kina na wa kitaalamu.
Akizungumza baada ya uchunguzi huo kukamilika, Kaimu Afisa Mahusiano wa Hospitali hiyo, Scholastica Ndunga, amesema madaktari bingwa walifanya uchunguzi wa kina na kubaini kuwa hakuna alama yoyote inayoashiria ukatili au tukio lililosababishwa na mtu.
“Tunaomba jamii iamini taarifa sahihi za kitaalamu. Uchunguzi wetu haukubaini chochote tofauti na madai yaliyokuwa yakisambazwa. Mwili wa marehemu uko katika hali ya kawaida kulingana na vigezo vya kitabibu,” amesema Ndunga.
Hata hivyo, ameongeza kuwa maamuzi na hatua zaidi kuhusu suala hilo zitatolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Vurugu zilizotokea zilisababisha uharibifu wa mali, ikiwemo kuchomwa moto kwa magari mawili aina ya Toyota Noah yenye namba T 350 DCH na Mazda CX-5 yenye namba T 214 EJU, huku watu kadhaa wakipata majeraha.
Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro wamezungumzia tukio hilo, wakisisitiza umuhimu wa wananchi kufuata sheria na kutoa nafasi kwa vyombo husika kufanya uchunguzi badala ya kuchukua sheria mkononi.
Juma Ally, mkazi wa Turiani, amesema tukio hilo ni la kusikitisha na linapaswa kuwa funzo kwa jamii.
“Ni sawa kuwa na mashaka, lakini si sahihi kutoa adhabu bila uthibitisho. Serikali na vyombo vyake vilipaswa kupewa nafasi ya kufanya uchunguzi bila vurugu,” amesema.
Naye Neema John, mkazi wa Manispaa ya Morogoro, amewataka wananchi kuacha kufanya maamuzi ya jazba yanayoweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo uharibifu wa mali na kuhatarisha maisha ya watu.
“Hata kama kuna maswali, sheria zipo, madaktari wapo na polisi wapo. Tukio hili liwe fundisho; tuache kuchukua sheria mkononi,” amesema.




