Taasisi ya Serikali ya uwekezaji wa pamoja (UTT AMIS) imesema mkakati wake mkubwa kwa sasa ni kusogeza huduma za uwekezaji karibu na wananchi kupitia matumizi ya teknolojia na upanuzi wa mtandao wa ofisi mikoani, hatua inayolenga kuwafikia Watanzania wengi zaidi ambao bado hawajanufaika na fursa za uwekezaji.
Akizungumza Desemba 19, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa UTT AMIS, Simon Migangala, alisema kuwa licha ya kuwepo kwa ongezeko la wawekezaji, bado kuna idadi kubwa ya Watanzania ambao hawajafikiwa, jambo linaloifanya taasisi hiyo kuongeza jitihada za utoaji wa elimu ya uwekezaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Migangala alieleza kuwa kupitia matumizi ya majukwaa ya mitandao ya simu na mfumo wa kidijitali wa portal, wawekezaji sasa wanaweza kuwekeza popote walipo bila kulazimika kufika ofisini, hatua inayolenga kuvunja vikwazo vya kijiografia na muda.

Aliongeza kuwa katika mwaka uliopita, UTT AMIS ilifungua ofisi mpya katika mikoa ya Morogoro na Kahama mkoani Shinyanga, kama sehemu ya mkakati wa kusogeza huduma za uwekezaji karibu zaidi na wananchi wa mikoa.






Kupitia maboresho hayo, Migangala alisema idadi ya wawekezaji wapya imeongezeka kwa kasi, ambapo zaidi ya wawekezaji 150,000 walijiunga ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, na kufanya jumla ya wawekezaji kufikia zaidi ya laki tano.
Alifafanua kuwa ukuaji huo umechangiwa pia na kuimarika kwa utendaji wa mifuko ya uwekezaji, ikiwemo Mfuko wa Umoja ambao umefikia thamani ya zaidi ya Sh bilioni 400, huku baadhi ya mifuko ikirekodi faida inayozidi asilimia 15.
Migangala aliongeza kuwa thamani ya jumla ya mifuko ya uwekezaji chini ya UTT AMIS ilifikia Sh trilioni 3.2 mwishoni mwa mwaka, ikilinganishwa na Sh trilioni 2.2 mwaka uliotangulia, hatua inayoonesha kuimarika kwa imani ya wawekezaji pamoja na ufanisi wa mifumo ya taasisi hiyo.






Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTT AMIS, Profesa Faustin Kamuzora, alisema taasisi hiyo ina jukumu kubwa katika kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kupitia kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala ya fedha na uwekezaji.
Profesa Kamuzora aliwataka waandishi wa habari kushirikiana na taasisi za kifedha katika kutoa elimu kwa umma, akisisitiza kuwa uwekezaji katika masoko ya mitaji ni nyenzo muhimu ya kuinua kipato cha Mtanzania na kufanikisha azma ya kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.









