Tuesday, December 16, 2025
spot_img
HomeHabariBalozi wa China: Uvumilivu na bidii ndio njia ya kuondokana na umaskini

Balozi wa China: Uvumilivu na bidii ndio njia ya kuondokana na umaskini

Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zinaweza kuondokana na umaskini endapo wananchi watakuwa na uvumilivu, ustahimilivu na kufanya kazi kwa bidii.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa toleo la Kiswahili la kitabu cha Rais Xi Jinping “Kupanda na Kutoka Kwenye Umaskini”, Balozi Mingjian alisema kitabu hicho kimeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya China na Mkuki na Nyota Publishers ili kutoa uzoefu na mbinu za kupambana na umaskini barani Afrika.

Kitabu hicho kimekusanya hotuba 29 na tafiti za Xi Jinping alizozitoa akiwa Katibu wa Chama cha Kikomunisti katika Wilaya ya Ningde, Mkoa wa Fujian (1988–1990), kipindi ambacho eneo hilo lilikuwa maskini zaidi nchini China. Kupitia mageuzi ya vijijini na sera shirikishi, maisha ya wananchi yaliboreshwa hatua kwa hatua.

Balozi Mingjian alisema mafanikio hayo yanaakisi falsafa ya maendeleo ya China yenye kumlenga mwananchi na imani ya Rais Xi katika kusaidia maeneo yaliyokuwa yamekumbwa na umaskini. Aliongeza kuwa China ilitimiza malengo ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza umaskini ya mwaka 2030 mapema kwa muongo mmoja, jambo lililoyapa matumaini mataifa mengi yanayoendelea.

Kwa mujibu wake, toleo la Kiswahili litakuwa daraja la mawazo kati ya China, Tanzania na Afrika kwa ujumla, huku kila nchi ikihimizwa kuchukua mafunzo hayo kwa kuzingatia mazingira yake.

Kwa upande wake, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alisema mapambano ya umaskini barani Afrika lazima yaanze kwenye fikra kwa kuondoa “umaskini wa mawazo,” huku kila jamii ikibuni suluhisho mahsusi kwa changamoto zake.

Naye Mkurugenzi wa zamani wa Mkuki na Nyota Publishers, Walter Bgoya, alisisitiza kuwa maendeleo yanahitaji viongozi wenye dira na uwajibikaji wa kuhamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii. Aliongeza kuwa msaada wa China katika kilimo, elimu na miundombinu, pamoja na uthabiti wa Tanzania, vinatoa fursa kubwa ya kupunguza umaskini.

Bgoya alihitimisha kwa kusisitiza kuwa uvumilivu, ubunifu na ushirikishwaji wa jamii ni nguzo kuu za Afrika kufanikisha maendeleo endelevu na jumuishi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments