Ile heshima na hadhi iliyokuwanayo Tanga miongo kadhaa iliyopita iko mbioni kurejea, baada ya Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan kuahidi kurudisha viwanda mkoani humo.
Kwa mujibu wa Dkt Samia, atakapochaguliwa kuiongoza tena Tanzania, atairudisha Tanga ya viwanda ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuifanya nchi kuwa na uchumi wa viwanda.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo jana, katika mkutano wake wa kampeni za urais, uliofanyika Tanga Mjini mkoani Tanga na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.
“Mwelekeo wetu wa ujumla ni kuirejesha ile Tanga ya viwanda, kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuijenga Tanzania ya viwanda kwa kuanzisha na kujenga kongani za viwanda kila Wilaya,” amesema.
Dkt Samia ameeleza Serikali yake itafufua viwanda vilivyobinafsishwa bila kuendelezwa, ikiwemo cha chai mjini Korogwe mkoani humo na kwamba amefurahishwa na hatua ya kufufuliwa kwa kiwanda cha foma.
Katika kufanikisha mkakati wa kuirudisha Tanga ya viwanda, amesema maeneo makubwa yasiyotumika lakini yanamilikiwa na watu, yarudishwe ili kutoa nafasi kwa watakaotaka kuwekeza kwa kujenga viwanda




