Monday, December 8, 2025
spot_img
HomeHabariSerikali yazindua mpango kutokomeza kichaa cha mbwa ifikapo 2030

Serikali yazindua mpango kutokomeza kichaa cha mbwa ifikapo 2030

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa afya ya wanyama imeandaa mpango rasmi wa kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa, ikiwa ni sehemu ya azma ya dunia ya kuondoa kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza leo, Septemba 29, 2025, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Kitaifa yaliyofanyika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, alisema mpango huo tayari umepitiwa na kuridhiwa na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH).

Alifafanua kuwa mpango huo unalenga kuhakikisha mbwa na paka wote nchini wanapatiwa chanjo ndani ya kipindi cha miaka mitano.

“Kupitia mpango huu, ni imani yetu kwamba hadi kufikia mwaka 2030 Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zitakazofanikiwa kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa,” alisema Meena.

Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana na wataalamu wa mifugo au serikali za mitaa pale wanapokutana na wanyama au mifugo wenye dalili zisizo za kawaida.

“Lengo la maadhimisho haya ni kukumbushana na kuelimishana zaidi jinsi ya kukabiliana na janga hili la ugonjwa wa kichaa cha mbwa,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Wanyama wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Benezeth Lutege, alisema kuwa mpaka kufikia Septemba 29, 2025, jumla ya mbwa 3,653 na paka 212 wamepewa chanjo wilayani Kiteto. Vilevile, mbwa 96 na paka 5 wamehasiwa, huku mbwa 52 na paka 26 wakifungiwa vizazi.

Akisoma taarifa ya Wilaya kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto, Bi. Mufandii Msaghaa, alisema serikali imekuwa ikitekeleza utoaji wa chanjo kwa mifugo na wanyama kama sehemu ya utekelezaji wa sera za mifugo na mkakati wa kuzuia magonjwa.

Maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Kitaifa kwa mwaka 2025 yamefanyika kwa kaulimbiu isemayo: “Kichaa cha Mbwa; Chukua Hatua Sasa, Mimi, Wewe na Jamii.”

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments