Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeHabariDkt Samia:Nitaifanya Mwanza kuwa jiji la kisasa zaidi

Dkt Samia:Nitaifanya Mwanza kuwa jiji la kisasa zaidi

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan, ameeleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayowezesha jiji la Mwanza kuwa la kisasa zaidi, tofauti na sasa.

Kwa mujibu wa Dkt Samia, miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na kumalizia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza ili uwe wa kimataifa na sambamba uboreshaji wa miundombinu ya masoko,maji na barabara zinazoingia ndani ya jiji hilo.

Dkt Samia ameeleza hayo, Jumanne Oktoba 7,2025 wakati akizungumza na wananchi wa Buhongwa, wilayani Nyamagana mkoani Mwanza aliposimama kuwasilimia baada ya kutua jijini humo, kuendeleza mikutano ya kampeni za kusaka kura kanda ya ziwa.

Katika maelezo yake, Dkt Samia amesema “Ndugu zangu najua ni kiu ya WanaMwanza, hili nilikuwa nilisema kesho, lakini nitalisema leo pia. Kiwanja cha ndege cha Mwanza, tunakikamilisha kuwa cha kimataifa ili kianze kazi,” ameeleza.

Dkt Samia amesema walikamilisha ujenzi wa barabara kutoka Buhongwa hadi Igoma yenye urefu wa kilomita 14 kwa Sh 22.7 bilioni, uliokwenda sambamba ujenzi wa madaraja ya Mikuyuni na Mabatini kwa gharama ya Sh 11.2bilioni.

“Tuliwaahidi kujenga barabara ya Mwanza hadi City Center, Buhongwa hadi Usagara kwa njia nne, niwaeleze zabuni imeshangazwa ili kumpata mkandarasi.

“Muda wowote fedha za kuanzia ujenzi, zikipatikana mradi unakwenda kuanza na Mwanza inakwenda kuwa jiji kweli kweli…Barabara nyingine zitakazojengwa ni Mkuyuni-Mahina-Mhandu hadi Igoma ambazo zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu,” amesema Dkt Samia.

Dkt Samia amesema ahadi yake kwa wananchi wa Mwanza ni kukamilisha miradi yote ya maji inayoendelea kutekelezwa ili kuboresha huduma kwa wakazi wa jiji hilo.

“Nafahamu kuna tatizo la presha kuwa ndogo baadhi ya maeneo hasa yenye miinuko, hivyo tunajenga matenki makubwa Nyamazobe (lita milioni tano), Buhongwa (lita milioni 10) na Fumagila ya juu (lita milioni 10),”

“Ujenzi wake umefikia asilimia 35, tutamaliza na mtiririko wa maji utakuwa mzuri na yatapatikana wakati wote kwa mwaka mzima,” amesema Dkt Samia huku akishangiliwa na wananchi wa Mwanza.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments