Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeHabariWenje:Ukisalimiwa jibu ‘Oktoba Tunatiki’

Wenje:Ukisalimiwa jibu ‘Oktoba Tunatiki’

Kada mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ezekia Wenje ametaka kauli ya ‘Oktoba Tunatiki’ iwe jawabu la salamu ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha Watanzania kujitokeza Oktoba 29 kumpigia kura mgombea wa CCM,Samia Suluhu Hassan.

‘Oktoba Tunatiki ‘ni kauli mbiu ya CCM inayotikisa kila kona ikilenga kuwahamisisha wanachama wa chama hicho na Watanzania kujitokeza kupiga kura na kumpigia Dk Samia.

Wenje ambaye alikuwa mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Victoria (Kagera, Geita na Mwanza), ametoa wito huo Jumatano Oktoba 15,2025 alipoitwa jukwaani kutoa salamu fupi katika mkutano wa hadhara wa kampeni za urais za Samia uliofanyika Muleba mkoani Kagera.

“Kama nilivyosema juzi, nikiwa Chato maisha yangu yote kwenye siasa nimekuwa nikicheza ndondo Cup, sasa nimekuja ligi kuu kucheza mpira mnene.Nyie WanaCCM mkitoka hapa (uwanjani), mtu akikusalimia habari za jioni we mjibu Oktoba tunatiki sawasawa.

“Kuanzia sasa salamu ibadirike ukisalimiwa habari ya asubuhi jibu ni Oktoba tunatiki,” amesema Wenje huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa kwanza, kwa Dkt Samia ambaye ameingia mkoa wa Kagera kusaka kura.

Kila alipokuwa akizungumza, Dkt Samia alionekana mwenye tabasamu na kumsikiliza kwa makini Wenje ambaye amesema wakati mgombea huyo anashika madaraka mwaka 2021, chama chake cha zamani kilikuwa na maombi mbalimbali ikiwemo kutaka mikutano ya hadhara ilifunguliwe.

Mbali na hilo, Wenje amesema kuna baadhi ya viongozi wa Chadema walikuwa wakiishi ughaibuni wakihofia usalama wao kutokana na kile kichotokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, hata hivyo, Dkt Samia aliyafanyia kazi.

“Tulikuwa na mahitaji yetu, tukaomba kuwa sisi tuliokimbia nchi turudi bila masharti, tulikuomba kwamba kulikuwa na watu wengi wa Chadema waliokamatwa baada ya uchaguzi wa 2020, lakini wote waliachiwa.

“Mheshimiwa mgombea urais uliruhusu mikutano ya hadhara ilifunguliwa, bahati mbaya tukaanza kukutukana, huku umeturuhusu kufanya mkutano.Uliunda kikosi kazi, lakini hatukuja tulisusa kama ilivyo kawaida yetu,lakini tulileta mapendekezo ya kutaka wakurugenzi nchi wasisimie uchaguzi,” ameeleza Wenje.

Wenje ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, amesema mapendekezo hayo yalifanyiwa kazi na Dkt Samia, akisema taarifa alizonazo hakuna wakurugenzi watakaosimamia uchaguzi wa Oktoba 29.

“Mheshimiwa mgombea tulipeleka mapendekezo kwamba hakuna mtu kupita bila kupingwa, sheria ilibadilishwa, leo hata kama mtu hana mgombea basi inapigwa kura ya ndio au hapana,” ameeleza Wenje.

Wenje ambaye ni mbunge wa zamani wa Nyamagana, pamoja na Rais Samia kutekeleza mapendekezo yaliyohitajika na Chadema, lakini chama hicho kilisusa uchaguzi jambo ambalo kada huyo amelifananisha na uoga na si vinginevyo.

“Tulisusa uchaguzi kwa uoga wetu, hiari yetu, kwa kuogopa ushindani, tukaweka mpira kwapani tukakimbia. Ukisoma biblia Mungu hafanyi kazi na watu waoga wanaogopa ushindani, sasa watu wanaokimbia ni hodari na shujaa?

“Mheshimiwa mwenyekiti ni hatari hapa duniani kuongozwa na mtu ambaye yupo tayari kufa, sasa huko nilikotoka kiongozi anakwambia yupo tayari kufa. Kiongozi ambaye yupo tayari kufa, huo ni uandawazimu,” amesema Wenje na kuibua kicheko kwa maelfu ya wananchi wakiwemo walioketi jukwaa kuu katika mkutano huo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments