Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeHabariTTB yajengea uwezo waongoza utalii wa utamaduni Mafia

TTB yajengea uwezo waongoza utalii wa utamaduni Mafia

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeandaa mafunzo ya siku tatu kwa waongoza utalii na viongozi wa serikali kisiwani Mafia, mkoani Pwani, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuanzisha na kuendesha vikundi vya Utalii wa Utamaduni (Cultural Tourism Enterprises – CTE).

Kisiwa cha Mafia kinatambulika kimataifa kwa vivutio vyake vya utalii wa baharini, fukwe na kuogelea na papa potwe (Whale Sharks). Hata hivyo, licha ya utajiri wake mkubwa wa kiutamaduni, fursa hiyo haijatumika ipasavyo kama zao la utalii linaloweza kuongeza mapato na ajira kwa wakazi wa eneo hilo.

Kutokana na umuhimu huo, wataalamu kutoka TTB, Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la WWF na WATONET, wameendesha mafunzo hayo ili kuwajengea washiriki uelewa wa namna bora ya kuendesha shughuli za utalii wa utamaduni kibiashara, kwa kuzingatia sheria na miongozo ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mafunzo hayo yameshirikisha viongozi wa vijiji vya Chole, Kilindoni na Kiegeani, na yamefanikisha kuanzishwa kwa vikundi vinne vya Utalii wa Utamaduni ambavyo ni Kilindoni CTE, Rasta House CTE, Tuyuli CTE na Rabiis Eco Cultural Tourism. Vikundi hivyo tayari vimesajili majina yao ya biashara katika BRELA kama hatua ya mwanzo kuelekea usajili kamili.

Mratibu wa Utalii wa Utamaduni kutoka TTB, George Mwagane, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada endelevu za serikali katika kukuza zao jipya la utalii wa utamaduni nchini. Alitoa wito kwa Watanzania kujivunia utamaduni wao na kuutumia kama fursa ya kujipatia kipato na kuunda ajira.

Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Amri Abdi, aliwahimiza waratibu wa vikundi hivyo kuzingatia misingi ya biashara na kuhakikisha ubora wa huduma wanazotoa kwa wageni, ili kuvutia watalii wengi zaidi kisiwani Mafia.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments