Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amesema kama ambavyo wananchi wanajitokeza kwa wingi kujaza mikutano yake ya kampeni, vivyo hivyo wajitokeze kupiga kura Oktoba 29, 2025.
Msisitizo huo wa Dk Samia, unakuja zikiwa zimesalia siku 11, kabla ya Watanzania kupiga kura za kumchagua Rais, wabunge na madiwani.
Dk Samia ameyasema hayo leo, Jumamosi Oktoba 18, 2025 alipozungumza na wananchi wa Kibaoni, mkoani Katavi katika mkutano wake wa kampeni za urais, uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Kwa kuwa siku zimebaki 11, amesema ikifika siku ya uchaguzi (Oktoba 29) kila aliyeandikishwa kwenye daftari la kupigia kura, aambatane na mwenzake kwenda kupiga kura.
Amerejea maelekezo yake kwa mabalozi wa mitaa, kuhakikisha kila mwananchi wa eneo lake anayestahili kupiga kura anakwenda kufanya hivyo.
“Naomba sana Oktoba 29, asilale mtu, kila aliyeandikishwa aende kupiga kura,” amesema.




