Kampuni ya Vodacom Tanzania PLC imezindua rasmi filamu ya “NIKO SAWA”, filamu ya kipekee ya Kitanzania inayopatikana kupitia VTV, jukwaa la kidijitali linalowezesha watazamaji kufurahia filamu na tamthilia mbalimbali kwa njia ya mtandao.
Uzinduzi wa filamu hiyo umefanyika leo katika ukumbi wa Cinema wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, ukiashiria hatua kubwa katika safari ya Vodacom ya kuwaunganisha Watanzania kupitia teknolojia na burudani zenye maudhui chanya ya kijamii.
Filamu ya NIKO SAWA inagusia kwa undani mada ya afya ya akili, ikieleza hadithi ya familia inayopambana na changamoto za kifedha, hisia na matatizo ya ndani yanayogusa maisha ya watu wengi. Uzinduzi wake umeenda sambamba na Maadhimisho ya Mwezi wa Uhamasishaji wa Afya ya Akili, ukilenga kuchochea mjadala kuhusu umuhimu wa kuelewa na kusaidiana katika changamoto za kiakili.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Idara ya Ubunifu wa Kidijitali wa Vodacom, Goodluck Moshi, alisema kuwa kupitia VTV, Vodacom inalenga zaidi ya burudani — inalenga kuelimisha na kuunganisha jamii kupitia hadithi zinazogusa maisha ya watu.

“Filamu ya NIKO SAWA ni hadithi yenye kugusa hisia, hasa kwa vijana. Inakumbusha kwamba afya ya akili ni muhimu kama afya ya mwili. Tunaamini teknolojia na sanaa ya usimulizi zinaweza kushirikiana kuleta mabadiliko halisi katika jamii,” alisema Moshi.
Kwa upande wake, Muongozaji wa filamu hiyo, Neema Ndepanya, alisema kuwa NIKO SAWA ni kazi ya sanaa iliyotoka moyoni, ikilenga kugusa mioyo na kuamsha mjadala kuhusu maumivu ya kimya kimya ambayo watu wengi hubeba bila kueleza.

“Kufanya kazi na Vodacom na kuona NIKO SAWA ikipata uhai kupitia VTV imekuwa safari yenye maana sana. Pale ambapo taasisi kama Vodacom zinawekeza kwenye hadithi za ndani, zinasaidia sanaa, zinaponyesha jamii na kutoa matumaini,” alisema Neema.

Wateja wanaweza kutazama NIKO SAWA na maudhui mengine ya VTV kwa kupakua bure programu ya VTV OTT kupitia Play Store au App Store, kisha kujisajili na kuchagua kifurushi cha bei nafuu kuanzia TSh 500 tu. Malipo yanaweza kufanywa kwa urahisi kupitia M-Pesa au njia nyingine za malipo ya simu.
Uzinduzi wa filamu hiyo unaashiria mwendelezo wa dhamira ya Vodacom ya kujenga maisha ya kidijitali yenye maana kwa Watanzania — maisha yanayowawezesha, kuwaburudisha na kuwaunganisha kupitia teknolojia, ubunifu na hadithi zinazogusa maisha halisi.





