Tuesday, December 16, 2025
spot_img
HomeHabariAgnes afariki kwa moto akijaribu kuokoa fedha za kikoba

Agnes afariki kwa moto akijaribu kuokoa fedha za kikoba

Mwanamke aitwaye Agnes James (33), mkazi wa Mwasele katika Manispaa ya Shinyanga, amefariki dunia kwa ajali ya moto baada ya kurudi ndani ya nyumba iliyokuwa ikiteketea kwa lengo la kuokoa fedha alizodaiwa kuchukua baada ya kuvunja kikundi cha vikoba.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa 9 usiku, wakati marehemu akiwa amelala pamoja na familia yake ndani ya nyumba yao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Afisa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, Edward Seleman, amesema walipopata taarifa na kufika eneo la tukio walikuta moto ukiwa umeshika kasi kubwa, huku mwanamke huyo tayari akiwa amefariki dunia ndani ya nyumba akiwa ameshika fedha mkononi.

“Tukio lilitokea majira ya saa 9 usiku. Tulipata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwasele B na kufika eneo la tukio, tukafanikiwa kuuzima moto, lakini Mama mwenye nyumba tulimkuta tayari ameshafariki,” alisema Seleman.

Alieleza kuwa awali marehemu alikuwa ameokolewa pamoja na familia nzima na mume wake na wote walikuwa nje ya nyumba. Hata hivyo, marehemu alirudi tena ndani kwa ajili ya kufuata fedha zake, ambazo inadaiwa alizipata baada ya kuvunja kikundi cha vikoba, kiasi ambacho bado hakijajulikana, ndipo moto ukamzidi na kusababisha kifo chake.

Seleman alisema baada ya uchunguzi wa awali, chanzo cha moto huo kimebainika kuwa ni hitilafu ya umeme. Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi kuhakikisha mifumo ya umeme, hususan katika nyumba za zamani, inafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara ili kuepuka majanga kama hayo.

Kwa upande wake, mume wa marehemu, Vicent Kilocha, alisema baada ya moto kuwaka alifanikiwa kuwaokoa watoto na wanafamilia wengine wote. Alieleza kuwa alitoka nje kwenda kuomba msaada kwa majirani, lakini aliporudi hakumuona mke wake.

“Nilipowauliza watoto waliniambia Mama amerudi ndani kuchukua hela zake. Moto ulikuwa mkali sana nikaona siwezi kurudi tena ndani kumuokoa,” alisema Kilocha kwa masikitiko.

Aliongeza kuwa walilazimika kusubiri hadi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilipofika na kuuzima moto, lakini mke wake alikuwa tayari ameshafariki dunia.

Nao baadhi ya majirani wa marehemu, akiwamo David Jonson, walisema walijaribu kuuzima moto huo mara walipofika eneo la tukio, lakini walishindwa kutokana na ukali wa moto na ukosefu wa vifaa stahiki, hali iliyosababisha kushindwa kumuokoa Mama mwenye nyumba.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments